August 05, 2014

  • TAIFA STARS NA MADOGO ZAO WA SERENGETI BOYS WATUA DAR, KAPOMBE AFUNGUKA KUHUSU MACHOZI YAKE!




    TAIFA STARS NA MADOGO ZAO WA SERENGETI BOYS WATUA DAR, KAPOMBE AFUNGUKA KUHUSU MACHOZI YAKE!
    Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
    TIMU mbili za Taifa za Tanzania, Taifa Stars na Serengeti Boys zimerejea Dar es salaam kwa ndege ya Air Tanzania kutokea Johannesburg nchini Afrika Kusini.Stars ilitokea Mjini Maputo na kuungana na wadogo zao nchini Afrika kusini na kusafiri pamoja leo.Kikosi cha Mart Nooij  jana kilifungwa mabao 2-1 na Msumbiji katika mchezo wa kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika, Afcon 2015 nchini Morocco.
    Mechi ya kwanza katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Stars ilitoka sare ya mabao 2-2 na Mambas na baada ya matokeo ya jana ilitupwa nje ya mashindano kwa wastani wa mabao 4-3.
    Kwa upande wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys yenyewe jumamosi Agosti 2 mwaka huu ilifungwa mabao 4-0 katika mchezo wa marudiano nchini Afrika kusini na kutupwa nje ya michuano ya kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana.
    Mechi ya kwanza uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, Serengeti walitoka suluhu ya bila kufungana na Amajimbos, hivyo matokeo ya jana yamewafanya watolewa kwa wastani wa mabao  4-0.
    Afisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania , TFF aliyeambatana na Taifa Stars nchini Msumbiji na kambi ya siku mbili Afrika kusini amesema kwamba timu zote zimewasili salama na kambi zote zimevunjwa rasmi leo hii.
    "Timu zote mbili zimerejea saa 9 alasiri kwa ndege ya Air Tanzania zikitokea Johannesburg Afrika kusini. Timu zote zilikuwa kwenye michuano ya Afrika, lakini kwa bahati mbaya zote zimetolewa na kambi zimevunjwa rasmi leo kusubiri programu nyingine za walimu." Alisema Wambura.
    "Kw utaratibu wa mpira, timu inapoingia kwenye mashindano, yanapokwisha au kuishia njiani, lazima benchi la ufundi likiongozwa na kocha mkuu litengeneze ripoti na kuiwasilisha sekretarieti, halafu inapelekwa kamati ya ufundi na kujadiliwa na baadaye inapelewa kamati tendaji na kuyafanyia kazi mapendekezo."
    Hata hivyo beki wa kulia wa Stars, Shomary Kapombe jana alimwaga machozi baada ya Stars kufungwa na baada ya  kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam alizungumza na waandishi wa habari.
    Kapombe alikiri kuumizwa na matokeo ya jana na kuwataka watanzania kutokata tamaa na timu yao.
    "Mchezaji kama mchezaji lazima uyapokee matokeo, lakini unaangalia tumefungwaje. Mechi ya Msumbiji matokeo kweli tumefungwa, lakini kuna vitu vinakatisha tamaa kama maamuzi ya refa.' Alisema Kapombe.
    "Katika mpira kuna changamoto, lakini napenda kuwaambia Watanzania kwamba wayapokee matokeo. Haikuwa nia yetu kufanya hivyo, tulienda kupigana ili kulinda matokeo, lakini tumefungwa, Watanzania wasife moyo, yatatokea  mashindano mengine tutafanya vizuri"

    "Nimejifunza kuwa Katika mashindano yoyote sasa hivi mchezo wa nyumbani ni muhimu zaidi. Nimeona tulivyokosa ushindi nyumbani, imetugharimu ugenini. Hili ni fundisho."


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.