Serikali inajipanga kufuta ada za sekondari, ili elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, itolewe bure.
Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo juzi katika mkutano wake na wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro, na wakazi wa vijiji vya jirani na chuo hicho, katika ziara yake inayoendelea katika Mkoa wa Morogoro iliyoanza Agosti 20.
"Sasa hivi tunaangalia jinsi ya kufuta karo katika shule zetu zote za sekondari za Serikali, ili kuhakikisha kila mtoto anayeanza darasa la kwanza, awe na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana ya kidato cha nne, bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada.
"Tunaangalia kuondoa ada hii, ambayo wazazi wanalipa Sh 20,000 kwa shule za kutwa na Sh 70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza, na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila wasiwasi wa kukwamishwa na ada," alisema Rais Kikwete.
Kwa hatua hiyo, Rais Kikwete alisema mbali na kulenga kuinua elimu, pia itawapunguzia mzigo wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule hizo za sekondari za Serikali.
Alisema zipo sababu za msingi zinazokwamisha wanafunzi wengi wa shule za sekondari, kuendelea na masomo yao kutokana na wazazi wao kushindwa kulipia karo ya shule, kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za umasikini.
Rais Kikwete alisema pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule za sekondari za kata, kiasi cha kuitwa Yeboyebo katika miaka ya mwanzoni ya shule hizo, bado zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya mafanikio ya Sekta ya Elimu katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.
Akielezea historia ya kuanzishwa kwa shule za sekondari za kata, Rais Kikwete alisema wakati alipokuwa akiingia madarakani, hali ya watoto kuingia sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa mbaya.Kwa mujibu wa Rais Kikwete, hali hiyo ilisababisha asilimia kati ya sita na kumi tu ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba, kusonga mbele kwa sababu shule za sekondari zilikuwa chache.
"Kwa miaka mingi, hatukujenga shule mpya za sekondari na kama mnavyojua, Wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata," alisema Rais Kikwete.
Alisema takwimu rasmi zinaonesha kwamba, kulikuwa na shule za sekondari 1,745 mwaka 2005, zikiwemo shule 1,202 za Serikali na sasa ziko shule za sekondari 4,576, zikiwemo shule 3,528 za Serikali.
Mafanikio hayo ya kupanuka kwa sekta ya elimu, kwa mujibu wa Rais Kikwete, yalileta changamoto hasa ya ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi. Alisema Serikali imepambana na changamoto hiyo na zingine zilizojitokeza, ambapo sasa wapo walimu karibu wa kutosha wa masomo hayo kwa shule za sekondari zote nchini.
Mbali na kusudio la kufuta ada, Rais pia alisema Serikali inaandaa utaratibu maalumu utakaowezesha kujenga mabweni katika shule za msingi na sekondari zilizopo maeneo ya jamii ya wafugaji.
Alisema lengo ni kuwawezesha watoto wa jamii hiyo, waendelee kusoma hata pale wazazi na walezi wao wanapohama kutoka eneo moja kwenda jingine kufuata malisho ya mifugo yao.
"Tuna tatizo kubwa katika eneo hili...watoto wengi wa wafugaji wanakatishwa masomo kutokana na wazazi ama walezi kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kufuata malisho...wanaohama wanaondoka na watoto wao wote na kuwakosesha fursa ya kusoma," alisema Rais.
Kuhusu elimu ya juu, Rais Kikwete alisema kwa sasa kuna vyuo vikuu 51, vikiwemo 15 vya umma na pia kuna ongezeko la fedha za mikopo ya elimu kutoka Sh bilioni 16 mwaka 2005 na kufikia Sh bilioni 345 kwa sasa.
Mbali na ongezeko la fedha za mikopo ya elimu ya juu, Rais Kikwete alisema wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu waliongezeka kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000 kwa sasa.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa, alipongeza Serikali kwa kukuza mitaala ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kushauri kuwa ili wanafunzi washindane katika soko la ajira, upo umihimu wa mitaala kuendelea kuboreshwa.
Alimwomba Rais Kikwete kusaidia kuboresha miundombinu mbalimbali ya chuo hicho kutokana na uchakavu wa majengo yake.
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Boniface Maiga, alitaja changamoto kubwa zinazowakabili kuwa ni pamoja na uhaba wa sehemu za malazi uliosababishwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaodahiliwa na uchakavu wa miundombinu.
Alisema licha ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), kutoa mikopo hiyo kwa wakati, bado kuna malalamiko mengi kuhusu watoto wa matajiri na wenye uwezo, ambao wameendelea kupewa mikopo.
Aliiomba serikali kufanyia utafiti suala hilo na ikibaini hali hiyo, fedha hizo zitolewe kwa watoto wengi masikini.
0 comments:
Post a Comment