August 26, 2014

  • ZOEZI LA UORODHESHAJI WA VIWANDA WILAYA YA LUDEWA LIMEANZA RASMI LEO


    ZOEZI LA UORODHESHAJI WA VIWANDA WILAYA YA LUDEWA LIMEANZA RASMI LEO
    Na Veronica Kazimoto,Ludewa

    Wito umetolewa kwa wamiliki wote wa viwanda waliopo katika wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe kutoa taarifa sahihi na ushirikiano wa kutosha kwa wadadisi wakaopita katika viwanda vyao ili kufanya zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Viwanda inayotarajia kufanyika mwezi Septemba, 2014.

    Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Iringa, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Meneja Takwimu mkoa wa Iringa na Njombe Fabian Fundi amesema zoezi hilo linaanza rasmi leo tarehe 25 Agosti, 2014 na litamalizika siku ya Jumapili tarehe 31 Agosti, 2014.

    "Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda wilaya ya Ludewa linaanza rasmi leo na litahusisha jumla ya kata kumi na sita ambazo ni pamoja na Ludende, Lugarawa, Ruhuhu, Lupanga, Lwela, Mavanga na Mundindi", amesema Fundi.

    Amezitaja kata nyingine kuwa ni, Ibumi, Mlangali, Kilondo, Madope, Lupingu, madilu, Makonde, Mkongobaki na Lifuma.

    Fundi amefafanua kuwa taarifa zinazokusanywa katika zoezi hili kutoka viwandani ni pamoja na jina la kiwanda, anuani za kiwanda, mahali kiwanda kilipo, aina ya umiliki na utaifa wa mmiliki.

    Taarifa nyingine ni gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mwaka kiwanda kilipoanzishwa, aina ya bidhaa zinazozalishwa, idadi ya wafanyakazi na gharama za uzalishaji.

    Zoezi hili la Uorodheshaji wa Viwanda lilianza tarehe 8 Aprili, 2014 kwa Tanzania Bara na mpaka sasa karibu maeneo yote zoezi hili limekwisha kamilika.
    Meneja Takwimu Mkoa wa Iringa na Njombe Fabian Fundi akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda limeloanza rasmi leo wilayani Ludewa kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Viwanda inayotarajia kufanyika mwezi Septemba, 2014.
    Meneja Takwimu Mkoa wa Iringa na Njombe Fabian Fundi akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika leo Mkoani Iringa kuhusu zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda limeloanza rasmi leo wilayani Ludewa kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Viwanda inayotarajia kufanyika mwezi Septemba, 2014. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO - LUDEWA)


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.