Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameungana na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, kuunga mkono mapendekezo ya Sheria ya Mgongano wa Maslahi.
Akizungumza jana wakati akifungua kikao cha kujadili mapendekezo ya kutungwa kwa sheria hiyo, Mkapa alisema mtumishi au kiongozi anayedhani kuwa sheria hiyo ni kandamizi, huenda akawa na tatizo la kutumia vibaya mamlaka ya umma.
Katika kikao hicho kilichojumuisha viongozi wa vyama vya siasa, makatibu wakuu, majaji na wakuu wa idara/vitengo vya sekretarieti ya maadili ya viongozi, Mkapa alisema sheria hiyo haimzuii mtu kupata, kumiliki au kuendeleza mali, ila kinachotakiwa ni kueleza namna ambavyo mali hiyo imepatikana.
"Sheria ya maadili ya viongozi wa umma ilianza kutumika nikiwa madarakani…wakati huo na hata sasa sikuwahi kuona tatizo la sheria hii," alisema Mkapa na kuongeza kinachosisitizwa ni ukweli na uwazi kwenye kuchuma mali, kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria.
Alisema ni ukweli kwamba Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ilianzishwa kwa lengo la kusimamia na kukuza maadili, hususani mienendo ya viongozi wa umma, lakini kadri siku zinavyokwenda anaona mienendo ya matumizi mabaya ya ofisi ikilalamikiwa.
Kadhalika alisema pia watumishi wa umma ambao siyo viongozi kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, nao wamekuwa wakilalamikiwa kwa hilo.
Mkapa alisema yamekuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, kuwa viongozi wao wamekuwa wakitumia vibaya rasilimali na madaraka waliyopewa na umma na kusababisha wananchi kupoteza imani waliyonayo kwa Serikali yao.
"Hoja zitakazotolewa zitajumuishwa pamoja na wadau wengine wa maadili, ili zitumike katika kuandaa waraka wa Baraza la Mawaziri ili kupata ridhaa ya kutunga sheria inayokusudiwa," alisema.
Mkapa alisema athari kubwa anayoiona katika Sheria ya Mgongano wa Maslahi, ni mtazamo hasi wa sehemu ya jamii juu ya kuweka kipaumbele katika maslahi ya umma.
Alisema katika hilo panahitajika kuelimisha umma, ili ubadili kwanza mtizamo huo, kwani endapo ikifanikiwa kazi itakuwa rahisi katika kujenga uchumi ambao ndani yake kuna ushindani wa haki na usawa.
Alisema jamii ni lazima ielewe kuwa misingi kisheria iliyowekwa, inakusudia kuimarisha amani na utulivu uliopo na sio kuwakandamiza wale wanaotumia nguvu zao kihalali katika kujipatia kipato.Mkapa alisema licha ya kuwepo mafanikio ya kuhakikisha maadili nchini yanazingatiwa, bado kuna tatizo lingine la kimaadili ambalo limeonekana nchini na kutopewa uzito unaostahili.
"Tatizo hili linajidhihirisha kwa namna ambavyo wenye mamlaka au watoa uamuzi wanapokuwa na maslahi kwenye jambo fulani, wanatumia madaraka waliyonayo katika kuendeleza maslahi yao binafsi badala ya kutoa kipaumbele kwa maslahi ya umma," alisema.
Alisema huo ndio mgongano wa maslahi ambao wengine huingia kwa makusudi au kutokujua na tatizo hilo linahitaji kutazamwa kwa umakini mkubwa.
Awali Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda, alisema hatarajii kupata malalamiko katika hali yoyote katika mchakato huo.
Alisema endapo viongozi waliopo madarakani watakasirishwa na sheria hiyo, hali hiyo watambue kuwa sheria ya maadili ya umma inawataka kutanguliza zaidi maslahi ya jamii mbele na kujichunga katika madaraka waliyonayo.
Aliyataja madhara ya mgongano wa maslahi kuwa ni uchumi kudidimia, wananchi kukosa haki zao za msingi kutokana na taasisi za umma kuendeshwa kwa misingi ya upendeleo, kuathiri mfumo wa uamuzi na michakato ya kidemokrasia, tofauti kubwa kati ya walio nacho na wasionacho na wananchi kupoteza imani na serikali yao.
Akizungumza wiki iliyopita, Mzee Mwinyi alisema Serikali haijawahi kufuta Azimio la Arusha, lililokuwa likidhibiti maadili ya viongozi kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi, bali ilizimua azimio hilo kuwapatia viongozi wa kati, uwezo wa kumudu makali ya maisha.
Lengo la kipato hicho kwa mujibu wa Mzee Mwinyi, ilikuwa kuwasaidia kumudu mahitaji ya maisha na kupata haki ya kikatiba ya uhuru wa kuwa na mali ya akiba ndogo, ili imuokoe mtumishi wakati wa dharura kama vile kuugua au kufiwa.
"Ninyi ni mashahidi kuwa hali hiyo ilikuwa kinyume cha matarajio, kwani watu wamekuwa wakitumia vibaya haki ile ya kikatiba, kwa kumiliki mali hata kwa njia zisizo halali… tuliwaruhusu kuingiza mkono, lakini wao wakaingiza mwili mzima," alisema.
0 comments:
Post a Comment