August 28, 2014

  • GENERAL DEFAO ALIVYOINUFAISHA KWAYA MAARUFU NCHINI



    KWA TAARIFA YAKO : GENERAL DEFAO ALIVYOINUFAISHA KWAYA MAARUFU NCHINI
     ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka maoni yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu.
    Uinjilisti Kijitonyama enzi hizo wakati mwimbaji huyo akiwa ndani ya kwaya.
    KWA TAARIFA YAKO hii leo ni kwamba kuna mwanamuziki wa nje ya kanisa aliyewika sana miaka ya 90's kutoka nchini Kongo zamani Zaire, huyu si mwingine bali General Defao Matumona, hapana shaka utakumbuka wakati wa umaarufu wake akapata mialiko ya kuja nchini kufanya maonyesho na onyesho lake la mwisho ambalo lilimwingiza matatizoni na kutorudi nchini mpaka leo ndilo ambalo GK inataka kugusia kidogo siku ya leo.

    KWA TAARIFA YAKO baada ya Defao kupata matatizo ya kuumwa na mambo mengine ya uhamiaji wakati alipoalikwa nchini kumbuka alikuja na timu ya wanamuziki wake ambao kutokana na mambo kuwa magumu walitawanyika kama kondoo waliyekosa mchungaji, na mmoja kati ya wanamuziki waliotawanyika anaitwa Joslii (jina aliko sahihi ila ndivyo alikuwa akifahamika) ambaye huko kwao Kongo ni mmoja kati ya waimbaji wanaoheshimika kwa uimbaji wa sauti za juu, yeye alienda kujiunga na kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama Lutheran ya jijini Dar es salaam ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikivuma sana, kwakuwa mwimbaji huyo alikuwa akiishi jirani kabisa na kanisa la Kijitonyama na akawa anawasikia Uinjilisti Kijitonyama wakifanya mazoezi mara kwa mara hivyo na yeye kujisogeza na kufanya mazoezi nao kisha kujiunga na kwaya.


    KWA TAARIFA YAKO Joslii maisha yake yalibadilika na kuamua kuokoka akiwa ndani ya kwaya hiyo ya Kijitonyama na kwakuwa alikuwa mwimbaji hodari aliweza kushirikiana vyema na waimbaji wengine na hatimaye kufanikiwa kurekodi album ya 'Twaokolewa kwa Neema' ya kwaya hiyo yeye akianzisha mapambio yakiwemo 'Twaokolewa kwa Neema, Toyelelo, Yehova Baba wa Upendo na mengineyo... utakubaliana nami kuwa mwimbaji huyo amejaliwa sauti nzuri ya juu na uimbaji wa ustadi. Ili kuendana sawa unaweza kusikiliza hizo nyimbo ili ujikumbushe. 

    KWA TAARIFA YAKO Joslii alifikia hatua ya kufunga siku tatu kavu bila kula chochote akimuomba Mungu juu ya maisha yake na huduma yake ya uimbaji kiasi kwamba alikuwa chachu hata kwa waimbaji wengine wa kundi la Kijitonyama Uinjilisti. Kwakuwa mwimbaji huyu anafahamika vyema nchini kwao Kongo, kumbuka pia hata Tanzania wakongo wapo hivyo basi wakaanza kumfuatilia na kuanza kumshawishi aachane na uimbaji wa kwaya na kujiunga na bendi za mziki wa nje ya kanisa, baada ya ushawishi wa muda mrefu wakafanikiwa na mwimbaji huyo kujiunga katika moja ya bendi ya muziki wa dansi.


    KWA TAARIFA YAKO kama neno lisemavyo katika kitabu cha Yohana 10:10 mwizi huja kwa nia ya kuiba, kuua na kuharibu… ndivyo hali ikaanza kumwendea kombo kwani alianza kutenda yale watendayo watu wa nje ya muziki wa kanisani hali iliyosababisha nduguze kutoka Kongo watume watu waje kumchukua kwakuwa bado wanamuhitaji katika ulimwengu wa muziki kitu ambacho walifanikiwa kuondoka naye ingawa GK haijui mwimbaji huyu anaendeleaje kwasasa.
    Uinjilisti Kijitonyama yasasa.
    KWA TAARIFA YAKO Joslii ndiye aliyeweka ushawishi mkubwa sana kwa kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama kutumia ngoma za live (drum) na sio zile za mshindo wa kutengeneza kwa kuwa hazipendezi kwa muziki wa live na kiwango cha kwaya hiyo kilivyokuwa. Unaweza kusoma taarifa nyingine kutoka kwaya hiyo kwa kubonyeza HAPA


    Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO vinginevyo tukutane wiki ijayo….


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.