Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Hirotaka Ishihara baada ya kukutana naye Ofisini kwake jijini Dar es salaam August 30, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema umefika wakati wa Japan kuhamia barani Afrika na na kuwekeza kwa nguvu hasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumamosi, Agosti 30, 2014) wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Bw. Hirotaka Ishihara na wafanyabiashara kutoka Japan kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Bw. Ishihara anaongoza ujumbe wa wafanyabiashara 70 kutoka makampuni makubwa 14 ya Japan.Akizungumza na Bw. Ishihara na baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo, Waziri Mkuu alisema ni ukweli usiopingika kwamba Japan ni nchi yenye uchumi imara na kwamba licha ya kuwepo kwa mikutano ya TICAD ambayo hutoa fursa kwa Japan kushirikiana na nchi za kiafrika, bado kuna haja ya wao kuelekeza macho yao Afrika kipekee.
"Mikutano ya TICAD imekuwa ikifanyika kwa zaidi ya miaka 20 sasa lakini nchi za Afrika na hasa Afrika Mashariki tumefumba macho… tumeshindwa kutumia kwa kiasi kikubwa fursa zilizopo na kuchota utaalamu wa kiteknolojia kutoka Japan," alisema.
Waziri Mkuu alisema Afrika Mashariki ni soko la uhakika kwa mtu yeyote anayetaka kuwekeza barani Afrika. "Kama nchi wanachama wa Jumuiya siyo soko la kutisha, lakini kutokana na mahali nchi zetu zilipo, tuna fursa kubwa ya kufungua milango ya soko kwa nchi zote jirani zinazotuzunguka na hiyo ni fursa kubwa kwa mwekezaji yoyote," alisisitiza.
Kuhusu uwekezaji, Waziri Mkuu alisema Japan inaweza kuwekeza kwenye viwanda vya nguo na kusokota nyuzi, kuna fursa kwenye viwanda vya kusindika samaki kwani kuna aina nyingi za samaki waliopo katika bahari ya Hindi. Pia alisema amefarijika kusikia kwamba wameonana na wahusika kutoka Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan ambaye ndiye kiongozi wa msafara huo alimweleza Waziri Mkuu kuridhishwa kwake na mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo mbili na kwamba katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na ongezeko la ziara za viongozi baina ya nchi hizi mbili.
"Nina furaha kuzuru Tanzania kwa mara ya pili nikiongoza Kamati ya Pamoja ya Umma na Sekta Binafsi ya Kukuza Biashara na Uwekezaji nchini Tanzania… tumevutiwa na kasi ya ukuaji uchumi wa Tanzania, ndiyo maana makampuni ya Kijapani yameonyesha nia ya kuja kuwekeza nchini Tanzania," alisema Bw. Ishihara.
Bw. Ishihara na msafara wake wamemaliza ziara yao ya siku ya tatu hapa nchini na wanaondoka Tanzania kurejea Japan leo jioni.
0 comments:
Post a Comment