Fatuma Misango mwenye mtandio mweusi kichwani akizungumza na mmoja wa wanawake waliotendwa.
-------------------------
Mwandishi HANNAH MAYIGE, wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania – OUT, anaangazia safari ngumu ya mwanaharakati mwanamke mzaliwa wa Namtumbo, Mratibu wa Kituo cha wasaidizi wa sheria Songea, Bi. Fatuma Misango katika harakati za kupigania haki za wanawake, watoto na kupinga ukatili wa kijinsia.
"Mimi naitwa Fatuma Misango, ni Mratibu wa kituo cha wasaidizi wa sheria kiitwacho Songea Paralegal Center (SOPCE)," Bi Fatuma alianza kujieleza kwa mwandishi wa makala haya ofisini kwake mjini Songea.
Bi. Fatuma Misango anasema yeye ni mzaliwa wa wilaya ya Namtumbo mkoa wa Ruvuma, mwenye umri wa miaka takribani hamsini sasa.
Anasema alikwama kuipata elimu yake kwa mfululizo enzi hizo kutokana na majukumu ya kifamilia, lakini aliamua kujiendeleza mwenyewe akiwa mtu mzima. Sasa ana elimu ya sekondari kidato cha nne inayomsaidia sana katika kutekeleza majukumu yake katika kuwasaidia wanawake, watoto na wanaume wenye uhitaji hasa wanaoteseka na ukatili wa kijinsia majumbani na sehemu za kazi
Kuhusu maisha, Mama Misango amejaliwa kuolewa na kupata watoto wanne na mume wake ambaye anaye mpaka sasa.Katika safari ya maisha yake alifanikiwa kufanya kazi kama karani katika Kampuni ya Tumbaku mjini Songea.
Hata hivyo, mama huyu , alikuwa anashauku na kiu ya kujiendeleza, hivyo aliamua kuanza masomo ya uuguzi ambapo alifanikiwa na kuhitimu masomo hayo kwa mwaka mmoja.
Bi. Misangu, hakuridhika na fani ya uuguzi tu, hivyo akajiingiza katika masuala ya siasa na kuwa Diwani viti maalumu kupitia CCM.
"Hapo ndio nikaanza kuangalia ni masuala gani ambayo nitaweza kusaidia jamii na hususani wanawake na watoto," anasema Bi. Misango na kufafanua kuwa baada ya hapo, "nikapata mafunzo ya sheria kama kiongozi yaliyoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali liitwalo Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TNGP) mwaka 2002,".
Mafunzo ya TGNP yalimpatia msukumo mkubwa na hamasa kuweza kuanza kuwasaidia wanawake kwa masuala ya sheria.
Bi. Misango anasema, wanawake wengi wakipata matatizo wanakuwa hawana pakwenda kueleza matatizo yao.
Shirika la TGNP linalosimamia mambo ya Jinsia na na kutetea haki za binadamu has masuala ya sheria walimwaalika tena kwenye semina jijjini Dar es salaam , baada ya kuona ana mwelekeo mkubwa katika uchangiaji wa mada mbalimbali hasa za utetezi wa wanawake.
Alipokuwa kwenye semina hiyo, ndipo alipokutana na maafisa wa Shirika ambalo lilimtaka washirikiane katika kazi ya kisheria au msaada wa sheria kwa wanawake katika mkoa wa Ruvuma , shirika hilo linaitwa Women Legal Aid Centre (WLAC)
Bi. Misango akaanza ukurasa mwingine wa kushirikisha watu wengine na kufungua Kituo cha wasaidizi wa Sheria Songea, Songea Paralegal Centre (SOPCE) kwa msaada mkubwa wa WLAC na yeye akiwa ni Mkurugenzi wake.
Walengwa wa Kituo hicho hasa, ni wale wa kipato cha chini ambao hawawezi kusimamiwa mashauri yao na Wakili kwa malipo ya fedha.Hivyo, walengwa wa jinsi zote awe mwanamke au mwanaume hupewa msaada na kituo hicho.
"Msaada wetu unakuwa ni bure, japokuwa lengo letu hasa ilikuwa ni wanawake na watoto zaidi," anasisitiza Bi. Misangu .
Shirika la SOPCE tangu lilipoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000, limeweza kuwasaidia watu takribani elfu tano (5,000).
Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Lihangweni, Songea Bi. Maria Komba, anatoa ushuhuda alivyosaidiwa na SOPCE. "Mimi ni mmoja wapo niliyepata msaada wa kisheria kutoka SOPCE baada ya kunyang'anywa ardhi na kijijii cha Lihangweni , na hatimaye nikarudishiwa ardhi yangu licha ya umasikini wangu unaonikabili," anasema Bi. Maria Komba .
Ushuhuda mwingine ni ule wa migogoro inayosumbua sana familia hasa ndoa. Bw. Dranus Tadei Njajula anasema bila msaada wa Mkurugenzi wa SOPCE, ndoa yake ingekuwa tayari imevunjika, lakini walimpatia msaada mkubwa sana na sasa ndoa yake imenusurika kuvunjika. "Hawa wamenisaidia sana kisheria, ndoa yangu sasa ni shwari" anajigamba Bw. Njalula.
Kwa kuona kazi nzuri SOPCE Na mkurugenzi wake Fatuma Misangu, serikali ya mkoa imekisaidia kituo hicho kwa kuwapatia ofisi bila malipo yoyote. Zaidi ya hapo wateja wengi wanatoka ofisi ya mkoa na ofisi ya wilaya ya songea vijijini.
Mama Misango alieleza kesi wanazo kutananazo zaidi ni kesi za ndoa "wanandoa wengi sana wana migogoro katika ndoa zao na mara nyingi sababu ni hali duni ya kiuchumi".
Kesi nyingine wanayo kutana nayo sana ni ukatili wa watoto "wanawake wanafanya ukatili kwa watoto wao kama kuwachoma moto mikono ukiuliza sababu eti kaiba shilingi mia mbili tu". Mama M isangu alibainisha kuwa sababu kubwa ni kuchoka maisha ya shida na mara nyingine kutelekezwa na waume zao, hivyo kupelekea msongo wa mawazo.
Mara nyingi hamna kazi au shughuli isiyo kuwa na faida na changamoto. "Nilipata tuzo ya amani 2005 iliyo julikana kama ONE THOUSAND PEACE WOMEN ACROSS THE GLOBAL. Kati ya watu elfu moja duniani waliopendekezwa basi na mimi nilikuwemo," anasema Bi Misango na kwamba faida nyingine ni kuwa maarufu.
Changamoto wanazo kabiliana nazo, ni pamoja na wateja wao wengi kuwa wa kipato cha chini, nao mara nyingi wanaamini pia kupata msaada wa fedha kutoka SOPCE. Changamoto hiyo inasumbua kwasababu shirika la SOPCE halina fedh za kuwahudumia watu kutatua matatizo yao.
Kuhusu malengo ya baadae, SOPCE inatarajia kuona jamii yote ya mkoa wa Ruvuma inaheshimu haki za binadamu hususan kwa wanawake na watoto. Pia wanataka wanawake wanasimama wenyewe katika kutetea haki zao.
Mama Misango alitoa ushauri kwa wanawake wajiunge katika vikundi mbalimbali vya ujasiriamali ili waweze kujikimu kimaisha. Kuishi bila kujishughulisha kuna sababisha kukata tamaa na wakati mwingine kuamua kufanya ukatili kwa watoto wao wenyewe .Biashara ndogondogo zinaweza pia kuwakwamua kimaisha .
Mwandishi wa makala anapatikana E-mail hannahmayige@gmail.com
0 comments:
Post a Comment