August 25, 2014

  • Madini Migodini yapo Salama- Maswi




    Madini Migodini yapo Salama- Maswi
    Na Asteria Muhozya, Mbinga

    Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amewataka watanzania kuondoa dhana kuwa madini yanayochimbwa katika migodi mbalimbali nchini yanaibwa na wawekezaji wakubwa na kusisitiza kuwa, Wizara kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), wapo katika migodi yote nchini kuhakikisha kwamba madini hayo hayatoroshwi .

    Maswi ameyasema hayo alipotembelea Mgodi wa kuchimba Makaa ya Mawe wa kampuni ya Tancoal eneo la Ngaka wilayani Mbinga inayomilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Australia na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na kuongeza kuwa, TMAA wapo katika kila mgodi kujua kiasi cha madini kinachochimbwa, kinachouzwa na kwa ajili ya kuhakiki vyeti vya mauzo ya madini hayo kuhakikisha kuwa vinakwenda sambamba na kiasi cha mrahaba kinachotolewa na wawekezaji.

    Kwa upande wake Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja alisisitiza hoja ya Katibu Mkuu Maswi na kuongeza kuwa, Wizara kupitia maafisa wa TMAA wamekuwa wakifanya ukaguzi kuhakikisha kwamba serikali inapata mrahaba stahili kupitia madini yanayouzwa na kutoa mfano kwa madini ya Makaa ya Mawe ya Ngaka kwamba serikali inapata asilimia 100 ya mrahaba.

    "Nawapongeza sana TanCoal ni wasikivu, maafisa wa TMAA huwa wanafanya ukaguzi kila baada ya miezi mitatu kujua kiasi kinachozalishwa na kinachouzwa hivyo, tunakwenda nao vizuri," alisisitiza Masanja.

    Naye Mkurugenzi wa Tancoal Tan Brereton ameeleza kuwa, mgodi wa wa Ngaka ni mradi mkubwa kwa Tanzania na kuongeza kuwa, uwepo wa mgodi wa makaa ya mawe wa Tancoal ni mafanikio na maendeleo makubwa kwa Tanzania kutokana na kuwezesha ajira kwa wataalamu mbalimbali nchini ikiwemo serikali kupata kodi na mirahaba kupitia mgodi huo jambo ambalo litawezesha kuboresha huduma za kijamii.

    Aidha, amezitaja faida za nyingine za mgodi huo kuwa, uwepo wa Mgodi huo utawezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha nishati ya umeme kutokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha makaa hayo katika mgodi wa Ngaka na kueleza kuwa, makaa ya mawe kutoka katika mgodi huo yana ubora wa kiwango cha juu tofauti na madini yanayochimbwa nchini Afrika Kusini.

    "Makaa ya Ngaka yana ubora wa hali ya juu sana tofauti na makaa ya nayochimbwa Afrika Kusini kwasasabu madini haya hayahitaji kusafishwa kabla ya matumizi tofauti na mengine ambayo husafishwa kabla ya kutumiwa ,alisisitiza Tan.

    Aidha ameongeza kuwa, kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani 480,000 za makaa ya mawe kwa mwaka na kuongeza kuwa, tayari kampuni hiyo imesaidia huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo ya afya,shule ,maji na kuwaendeleza vijana na kutumia zaidi ya shilingi milioni mia sita na kuongeza kuwa, kampuni hiyo imekwisha toa kiasi za bilioni 2 kama kodi na mrahaba kwa serikali.

    Kwa mujibu wa Tan, ameeleza kuwa, makaa yanayozalishwa na kampuni hiyo yanatumika katika viwanda vya saruji vya Mbeya Tanga Lake, kampuni ya METL na viwanda vya karatasi viwanda vya nguo.
    Mashine ya kusaga makaa yam awe katika viwango mbalimbali kulingana na mahitaji ya wateja ikiendelea na kazi ya kusaga mawe katika Mgodi wa Mkaa ya Mawe wa Ngaka unaomilikiwa kwa ubia na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na kampuni ya Australia.
    Gari la kubeba makaa ya Mawe katika mgodi wa Ngaka likimwaga makaa sehemu maalum kutoka mgodini kabla ya kusagwa katika viwango mbalimbali kulingana na mahitaji y wateja.
    Meneja wa Kampuni ya TANCOAL (wanne kulia) Tan Brereton na Mkuu wa Masoko wa kampuni hiyo Emmanuel Constantinides (wa tatu kulia) wakimwonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi na ujumbe wake namna shughuli za himbaji Makaa ya Mawe zinavyofanyika.
    Gari la kubeba kupakia Makaa ya Mawe likiendelea na kazi hiyo katika Mgodi wa Ngaka unaomilikiwa na kampuni TANCOAL.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.