August 29, 2014

  • Wataalam Ngazi ya Kata kutumika kupunguza Athari za Maafa ya Ukame


    Wataalam Ngazi ya Kata kutumika kupunguza Athari za Maafa ya Ukame
    Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa imesema itawatumia Wataalam waliopo katika Ngazi ya Kata katika Mradi wa kuzijengea uwezo jamii wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame. Kauli mbiu ya Mradi huo ni "Athari za Ukame Zinapunguzika, Jamii ikielimishwa."

    Akiongea wakati wa Mafunzo juu ya Utekelezaji wa Mradi huo kwa Wataalam wa Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala wa kata ya Hedaru, Makanya na Vunta, Wilayani Same, Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Mradi huo Bw. Harrison Chinyuka alifafanua kuwa lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea Uwezo wataalam hao wa kutambua viashiria na vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa ili waweze kutoa elimu sawia kwa vikundi vinavyotekeleza mradi huo katika kata zao.

    "Kutokana na mabadiliko ya Tabia Nchi yameleta athari nyingi ikiwemo ukame, kupitia mradi huu ulioanza kutekelezwa kwa majaribio katika Wilaya ya Same hasa katika Kata ya Hedaru, Makanya na Vunta, hivyo wataalam kupitia mafunzo haya wataweza kuvieimisha vikundi vya kata zao husika juu ya kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame." Alisema Chinyuka.

    Chinyuka alifafanua kuwa Wataalamu hao katika ngazi ya kata ndio waratibu katika kuijengea jamiii uwezo wa kukabiliana na kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa ya ukame kwakuwa Wataalam hao hutoa mafunzo kwa wadau kuhusu matumizi ya mbegu na pembejeo za kilimo, mifugo na misitu pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

    Wakitoa mada wakati wa mafunzo hayo Wakufunzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika walibainisha kuwa Wataalam katika Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala wa kata ya Hedaru, Makanya na Vunta wanalo jukumu la kuelimisha jamii juu ya matumizi ya Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini pamoja na Umuhimu wa Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe Nchini katika kata zao.

    Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo Afisa Mtendaji Kata Hedaru, Bw. Jackson Mbwambo alibainisha kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wataalam wa ngazi ya kata wa kuweza kupunguza athari za maafa ya ukame na kuahidi kushiriki kikamilifu katika kuijengea jamiii uwezo wa kukabiliana na kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa ya ukame katika kata zao.

    Mikoa ya Kilimanjaro na Shinyanga ndio inayotekeleza mradi huo, wilaya zinazoshiriki katika mradi huo ni pamoja na Same, Hai na Mwanga kwa mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya za Kishapu, Shinyanga Vijijini na Shinyanga Mjini kwa mkoa wa Shinyanga.

    Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa Kwa Mikoa Iliyoathirika Zaidi Na Ukame umefadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Halmashauri husika wakiwa Watendaji Wakuu wa Mradi huo. Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi uliozinduliwa Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba2013.
    Baadhi ya Wataalam katika Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala wa kata ya Hedaru, Makanya na Vunta Wilayani Same, wakinukuu masuala muhimu wakati wa mafunzo ya jinsi ya kutekeleza Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo wa kupunguza Athari Za Maafa katika kata zao, mafunzo hayo ya muda wa wiki moja yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.