Na John Gagarini, Kibaha
WANAWAKE nchini wametakiwa kutokubali kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuhofia kutengwa na familia zao badala yake wawe watoa taarifa ili kuwadhibiti watu wanaoendeleza vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria na uvunjaji wa haki za binadamu.
Tabia ya kuficha ukatili wa kijinsia imesababisha wahusika kujikuta wakiathirika kutokana na vitendo hivyo ambavyo vimeshamiri kutokana na kuendelea kwa usiri ndani ya familia.
Hayo yalisema jana mjini Kibaha na mkurugenzi wa benki ya Wanawake Tanzania Magreth Chacha, wakati wa uzinduzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Pwani (PWMO).
Chacha alisema kuwa baadhi ya wanawake wamekuwa wakificha vitendo hivyo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wanaume wasiokuwa na huruma.
"Vitendo vya ukatili wa kijinsi vimekuwa vikifanywa ndani ya familia huku wanawake amabao ndiyo wahanga wa matukio hayo wamekuwa wakikaa kimya kuhofia kutengwa na familia zao jambo ambalo limesababisha vitendo hivi kuendelea," alisema Chacha.
Alisema kuwa baadhi ya vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na watu wa karibu wa familia wakiwemo wanandoa na ndugu hali ambayo inasababisha taarifa hizo kufichwa huku walengwa wakiendelea kuathiriwa na vitendo hivyo viovu na vya ukatili.
"Baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na wanawake kupigwa, kutumikishwa kingono, kubakwa, watoto kubakwa, kulawitiwa, kufanyishwa kazi licha ya kuwa na umri mdogo na vitendo vingine vinavyokwenda kinyume cha sheria na haki za msingi za binadamu," alisema Chacha.
Kwa upande wake mwenyekiti wa (PWMO) Mwamvua Mwinyi alisema kuwa lengo la kuanzishwa chama hicho mbali ya kutetea haki za waandishi wanawake pia ni kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
"Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku kutokana na baadhi ya wanajamii hususani wanawake kutokuwa katika kutoa taarifa za vitendo hivyo hali inayofanya kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia," alisema Mwinyi.
Aliiomba jamii kwa kushirikiana na vyombo vya sheria kwa kutoaa taarifa juu ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili hususani maeneo ya pembezoni mwa miji, chama hicho kilianzishwa mwaka jana na kina jumla ya wanachama 15.
0 comments:
Post a Comment