August 27, 2014

  • China yaungana na Tanzania kutokomeza uhalifu




    China yaungana na Tanzania kutokomeza uhalifu
    Na Tamimu Adam – Jeshi la Polisi

    Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekabidhiwa msaada wa vifaa vyenye thamani zaidi ya milioni mia moja kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa ajili ya matumizi ya ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Mambo ya ndani na ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi Tanzania.

    Msaada huo, ulitokana na Ziara ya Naibu Waziri wa Usalama wa raia wa Jamhuri ya watu China aliyoifanya hapa nchini mwezi mei mwaka jana ambapo aliahidi misaada mbalimbali kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi.

    Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa na Balozi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini Mhe. Xu Youqing kwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Pereira Silima ni pamoja na Kompyuta Thelasini (30), Viti tisini na mbili (92), Meza hamsini (50) na PA System kwa ajili ya kumbi mbili za mikutano.

    Aidha, Balozi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini Mhe. Xu Youqing alikabidhi Pikipiki hamsini (50) kwa Jeshi la Polisi ambazo zilipokelewa rasmi na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Silima. Pikipiki hizo zilitolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya watu wa China kwa niaba ya jumuiya ya wafanyabiashara wa kichina walipo Afrika wakati wa ziara yake aliyoifanya hapa nchini mwezi juni mwaka huu.

    Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe. Pereira Silima baada ya kupokea vifaa hivyo, alimshukuru Balozi huyo wa China na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China Pamoja na Wafanyabiashara wa Kichina waliopo Afrika kwa msaada walioutoa kwa Serikali ya Tanzania, na kueleza kuwa vifaa hivyo vyote vitakuwa ni chachu katika kuzuia, kupambana na kukabiliana na uhalifu hapa nchini.

    Naye, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki alisema kuwa mbinu za kutenda uhalifu hubadilika mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia, na katika kukabiliana na mabadiliko hayo Jeshi la Polisi liko kwenye utekelezaji wa Maboresho yaliyojikita katika mihimili mikuu mitatu ambayo ni kulifanya Jeshi kuwa kisasa, lenye weledi na linaloshirikiana na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu, hivyo vifaa vilivyokabidhiwa vitalisaidia Jeshi la Polisi katika mpango huo unaolenga kuzuia uhalifu.
    Balozi wa Jamhuri ya watu wa China akipokea cheti kinachoonyesha ushirikiano mzuri baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Pereira Silima wakati wa kukabidhi msaada wa kutoka Serikali ya watu wa China.
    Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi , Mhe. Pereira Silima amekaa juu ya pikipiki,(kushoto kwake) Balozi wa China hapa nchini Mhe. Xu Youqing (kulia) (katika) Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi,Abdulrahman Kaniki wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa vya ukumbi , pikipiki pamoja na kompyuta zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Picha na Hassan Mndeme- Jeshi la Polisi.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.