UMOJA wa Katiba ya Wananchi              (Ukawa), umemtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe              (Chadema), kuacha kuwaingilia kwenye mambo kwa vile              hayamhusu.Kauli ya Ukawa imekuja siku moja baada ya Zitto              kusema hana uhakika na wala haamini kama umoja huo utakuwa              endelevu hadi uchaguzi mkuu mwaka 2015, kwa sababu si mara              ya kwanza vyama vya upinzani kuungana kisha              kugawanyika.Alisema siku zote Watanzania wanapenda kuwa na              upinzani imara ambao watu wanaweka maslahi yao pembeni na              kuungana dhidi ya chama kilichopo madarakani.Akizungumza na              MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha              Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa,              alisema haoni umuhimu wa kujibizana na mtu aliye nje ya              umoja huo kwa sababu hawezi kujua dhumuni la kuungana.
          "Hatuhitaji              kuumiza kichwa wala kujibizana na mtu aliye nje ya Ukawa,              kwa sababu hajui ulianzishwa kwa lengo gani, atabaki              kutabiri kitu ambacho hana uhakika nacho, bali anazungumza              kutokana na matakwa yake.
        "Kwanza              si msemaji wa Ukawa, tunashangaa hata kukaa na kuanza              kujadili suala lisilomhusu, ni nani na ninyi waandishi wa              habari mnapaswa kumuuliza maswali wakati akizungumza hayo,"              alisema Dk. Slaa.
        Alisema              Ukawa haufanyi kazi kwa kufuata maneno ya barabarani, bali              wanafanya kazi kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kusikiliza              maoni ya wananchi nini wanataka ili waweze kuyafanyia kazi.
        Alisema              tangu kuanzishwa kwa umoja huo, wamekwenda zaidi ya mikoa 17              na majimbo yake ili kusikiliza maoni ya wananchi ambayo              wameyachukua na kuyafanyia kazi, hivyo basi hawana muda wa              kukaa na kujadili kauli za watu zinazotolewa barabarani za              kujadili masuala yasiyowahusu.
        "Sisi              tunafanya kazi na Watanzania, hatufanyi kazi na mtu mmoja              mmoja, ndiyo maana tulikwenda mikoa 17 na majimbo yake kwa              ajili ya kuwaelezea umoja wetu na mikakati tuliyopanga ndani              ya umoja huu, hivyo basi hatuna nafasi ya kujadili kauli ya              mmoja mmoja," alisema.
        Alisema              kutokana na hali hiyo, viongozi wa umoja huo hawawezi kuishi              kwa imani, bali wanafanya kazi kwa vitendo ili wananchi              waweze kuwahukumu katika uchaguzi ujao.
        Alisema              Ukawa haupo kwa ajili ya Katiba peke yake, bali ni kuangalia              maslahi ya wananchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na              kijamii ili kuhakikisha wanaondokana na hali ngumu ya maisha              na kupata mafanikio.
        Alisema              mkakati uliopo ni kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kwa              vitendo ili wananchi wenyewe waweze kuwanyooshea vidole              kwenye chaguzi zijazo.
        Naye              Katibu wa Ukawa ndani ya Bunge, Julius Mtatiro, alisema              mawazo ya mtu yanapaswa kuheshimiwa, lakini umoja huo              hauwezi kufanya kazi ya utabiri kama utaendelea au              kuvunjika.
        "Ukawa              hauwezi kufanya kazi ya utabiri, kwa sababu tulipoungana              tulikuwa na malengo ya dhati, ikiwa ni pamoja na kuondoa              tofauti zetu na kuangalia maslahi ya wananchi na si kauli ya              mmoja mmoja, japo naheshimu mawazo yake," alisema Mtatiro.
        Mtatiro              alitolea mfano kwa kusema kauli ya Zitto ni sawa na falsafa              ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo wamekuwa wakitangaza              kila kona kuwa upinzani Tanzania unaelekea kufa wakati si              kweli.
        WAJUMBE
        Katika              hatua nyingine, Ofisi ya Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba              imewataka wajumbe wa Bunge hilo kuwasili Dodoma Agosti kwa              ajili ya kuanza mkutano huo kama ulivyopangwa.
        Taarifa              iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam na              ofisi hiyo, ilisema Bunge Maalumu la Katiba linatarajia              kuanza vikao vyake Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.
        Taarifa              hiyo ilisema Agosti 4 itakuwa siku maalumu kwa ajili ya              mambo ya kiutawala, hivyo wajumbe wote wanapaswa kufika              Ofisi za Bunge Dodoma kuanzia saa 4:00 asubuhi.
        
0 comments:
Post a Comment