December 30, 2015

  • WAZIRI WA FEDHA AFICHUA MAZITO JUU YA SAFARI ZA KWENDA KUOMBA MSAADA NCHI ZA NNJE


    WAZIRI WA FEDHA AFICHUA MAZITO JUU YA SAFARI ZA KWENDA KUOMBA MSAADA NCHI ZA NNJE

    Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema serikali inatarajia kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 1.3 ndani ya mwezi huu pekee.


    Aidha, amesema ili kuhakikisha serikali inapata mapato ya kutosha, atasimamia vyema suala la kukusanya kodi zinazostahili na kutengeneza mazingira ya watu kulipa kodi.

    Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya Ikulu mara baada ya kuapishwa, Dk. Mpango alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja serikali inaweza kukusanya kiasi hicho cha fedha.

    "Nimekaa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kipindi cha wiki tatu, nimeona kuwa kiasi hiki cha Sh. trilioni 1.3 kinaweza kukusanywa. Kwa wiki iliyopita ya sikukuu, niliona makusanyo ni mazuri na mpaka ifikapo mwisho wa mwezi huu, tutatimiza kiasi hicho," alisema.


    Namna ya kukuza Uchumi wa Nchi
    Dk. Mpango, alisema ili kukuza uchumi wa nchi ni lazima kuwa na utaratibu wa kujenga viwanda vikubwa nchini vinavyozalisha kwa wingi  jambo litakaloongeza pato la taifa.

    "Nchini kwa sasa kuna kiwanda kimoja kikubwa cha Bia cha Breweries (TBL) ambacho ndicho tunakitegemea ndio maana bei ya vileo vinapanda kila siku. Lakini vingekuwapo kama hivyo 10, nina uhakikisha tungekusanya mapato ya kutosha," alisema.

     Aibu ya kuomba misaada nje
    Dk. Mpango, alisema miongoni mwa mambo yanayomnyima raha ni safari za kwenda ughaibuni kuomba misaada kwa nchi wahisani.

    Alisema kitendo hicho ni cha aibu na kwa muda mrefu kimekuwa kikimsonesha moyoni hasa kwa kuwa anafahamu kuwa taifa lake lina utajiri mkubwa.

    "Nimekwenda nje mara nyingi nikiongozana na mawaziri wa fedha waliopita kwenda kuomba misaada.Huwa najisikia aibu sana,tunadhalilika sana. 
     
    "Hatuna sababu ya kuwa ombaomba,tunachotakiwa kukifanya ni kuimarisha mfumo wa ukusanyaji kodi na kuwaondolea mzigo wananchi wa hali ya chini," Alisema Dr. Mpango


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.