December 03, 2015

  • RAIS WA ZANZIBAR DK SHEIN AGEUKWA NA WAPAMBE WALIOMSHAWISHI AGOMBEE URAIS



    RAIS WA ZANZIBAR DK SHEIN AGEUKWA NA WAPAMBE WALIOMSHAWISHI AGOMBEE URAIS
    Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema baadhi ya wapambe na vigogo waliompigia debe na kumshawishi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, achukue fomu kuwania urais kwa mara ya kwanza mwaka 2010, hivi sasa wamemgeuka na baadhi yao wanamuona kikwazo kutokana na msimamo wake wa kimapinduzi usioyumba, wala kuogopa vitisho katika kuweka maslahi ya umma mbele.
    Akizungumza wakati alipokutana na makundi ya vijana wa CCM kutoka majimbo manne visiwani hapa jana ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi wa marudio Zanzibar, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema watu hao walitarajia Dk. Shein baada ya kuwa Rais angekuwa dhaifu, mwepesi na angekubali kutii na kushiriki usaliti dhidi ya uhuru na mapinduzi kwa manufaa ya wachache, lakini imeshindikana kutokana na Rais huyo kuweka mbele maslahi mapana ya Zanzibar na wananchi wake.
    "Madalali hao wa kisiasa hawakujua wala kufahamu kama Dk. Shein ni zao la mapinduzi. Laiti kama Dk. Shein asingelelewa, kuandaliwa na kukuzwa chini ya misingi ya kimapinduzi, waliopania kuyatokomeza mapinduzi yetu wangepata mwanya wa kuukwapua urithi huo na kuturudisha nyuma kama ilivyokuwa enzi za utawala wa sultani ambao wengi walidhalilika na wachache kuneemeka," alisema.
    Shaka aliwataka Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti za itikadi za kisiasa kuendelea kumuunga mkono Dk. Shein, kwani anasimamia maslahi ya Zanzibar na wananchi wote ili Zanzibar iwe mahali bora na salama pa kuishi kwa kila mtu.
    "Naona fahari kukitumikia chama changu nikiwa bado kijana, nakomazwa, kufunzwa na kuelimishwa ili kujua pumba na mchele. Wanaojifanya vinara wa uongo nawasikitikia kwa sababu watamalizika kisiasa kwa aibu," alisema.
    Aidha, Shaka aliwataka vijana, wajumbe wa nyumba kumi na wana maskani wa CCM kuamka na kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa marudio kabla ya kutangazwa kwa tarehe rasmi ya kufanyika uchaguzi huo.
    Kwa upande wao, vijana hao walimueleza Shaka kwamba wapo imara kuyalinda na kuyatetea mapinduzi ya Zanzibar na kwamba wanachohitaji ni kuwa na viongozi wanaotenda kulingana na kauli zao.
    Shaka yuko katika ziara ya kukutana na makundi ya vijana, wanawake, wazee na wajumbe wa nyumba 10 visiwani Zanzibar. ikiwa ni mkakati wa kuimarisha UVCCM na CCM kwa jumla katika majimbo yote 54 ya visiwa hivyo kabla kuingia katika uchaguzi wa marudioa.


    CHANZO: NIPASHE


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.