Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imeingilia kati mgogoro wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa kuwasimamisha kazi Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Nassoro Baraza na Naibu Meneja Mkuu, Samweli Swai ili kupisha uchunguzi dhidi yao ufanyike na endapo watabainika kuwa ni chanzo cha mgogoro huo watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, serikali imetoa miezi sita kwa kiwanda hicho kiwe kimewalipa wafanyakazi madai yao mbalimbali sambamba na kuanza kulipa nyongeza ya mishahara wanayodai kama sehemu muhimu ya kumaliza kabisa mgogoro huo.
Akitoa agizo hilo jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Uledy Mussa, alisema serikali imeona ni vema kufanya maamuzi magumu kwa mtu mmoja au wawili ili kunusuru uwapo wa nguvu kazi nyingi hasa kwa watu wanaohitaji kutimiziwa haki zao za msingi.
Uledy pia alikitaka kiwanda hicho kuwalipa wafanyakazi wote kiwango kipya cha mishahara yao ya Sh. 150,000 ifikapo mwishoni mwa Desemba mwaka huu, kama wizara ya kazi na ajira inavyosema kupitia mwongozo wa mishahara ya wafanyakazi nchi.
Licha ya hayo, pia Uledy alisema serikali ipo katika hutua za mwisho kutafuta muwekazaji mpya katika kiwanda hicho ambaye atahakikisha analinda maslahi ya wafanyakazi na taifa kwa ujumla.
"Hatua hiyo ni muendelezo aliokuwa akifanya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Marehemu Dk. Abdallah Kigoda,"alisema Uledy.
Pamoja na madai mengine, wafanyakazi hao pia wanahitaji kujua hatma ya wastaafu kulipwa Sh. 200,000 mara baada ya kustaafu, jambo ambalo Uledy alihitaji muda tena kabla ya kutoa jibu kamili kwa madai kwamba hakuwa na uwezo wa kulitolea ufafanuzi kwa wakati huo.
Katika hatua nyingine wafanyakazi wa kiwandani hicho wamemtaka Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (Tuico), Florian Makero, kujihuzulu wadhifa huo kwa kile kunachodai kuwa ameshindwa kuwatetea katika kutafuta haki zao kuwa upande wa uongozi.
0 comments:
Post a Comment