Watuhumiwa wa dawa za kulevya waliopo katika magereza mbalimbali likiwamo la Keko jijini Dar es Salaam, wamemuomba Rais Dk. John Magufuli (pichani) , kuwasaidia ili kesi zao zisikilizwe kwa kuwa wamekaa jela kwa zaidi ya miaka minne. Kwa mujibu wa barua waliyoandika kwa Rais Magufuli na Nipashe kupata nakala yake, kwa zaidi ya miaka minne wamekuwa wakipelekwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam bila kesi zao kusikilizwa.
Hata hivyo, wamesema licha ya kupelekwa mahakamani kila baada ya wiki mbili, lakini kesi zao hazijawahi kusikilizwa kwa madai kwamba upelelezi haujakamilika, majalada yao yamepotea, ama yana makosa.
"Kufungwa ama kuachiwa, ni haki yetu ya msingi na tumebaini kuwapo kwa njama chafu za kuendelea kutushikilia gerezani bila kesi zetu kuanza kusikilizwa," ilidai sehemu ya barua yao.
Watuhumiwa hao wamesema kuendelea kukaa gerezani kwa zaidi ya miaka minne ni hasara kwa serikali kwa kuwa kipindi chote hicho wanakula bure kutumia fedha za umma ukiachilia mbali kuwa mbali familia zao kukosa huduma kutoka kwao.
Kupitia barua yao wamedai kwamba ni watuhumiwa na dawa za kulevya katika magereza yaliyopo Mkoa wa Dar es Salaam, wamelalamikia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa madi kwamba ina utendaji mbovu.
Walisema katika barua yao kwamba kuna watuhumiwa wamekiri kuhusika na dawa hizo, lakini bado serikali inasema upelelezi haujakamilika.
Kutokana na kero na usumbufu wanaoupata watuhumiwa hao, wametangaza mgomo wa kutoshuka katika gari la mahabusu watakapopelekwa mahakamani kushinikiza kesi zao zianze kusikilizwa.
Wamelalamika kwamba wenzao mwaka jana walipogoma kula wakidai kesi zao kusikilizwa, hakimu aliamua kuwahukumu kwa hasira na kila mmoja alihukumiwa miaka 30 jela. Walisema mahakama itende haki na isitoe hukumu kwa hasira kwa kuwa kesi zao kuanza kusikilizwa ni haki yao ya msingi. Waliongeza kuwa wameandika barua za malalamiko katika taasisi nyingi za serikali, lakini hakuna anayewasikiliza mpaka sasa na kwamba mtu pekee ambaye wanaamini atawanusuru ni Rais Dk. Magufuli.
NIPASHE.
0 comments:
Post a Comment