December 22, 2015

  • Malope kuwasili Alhamisi wiki hii tayari kwa Tamasha la Krismasi



    Malope kuwasili Alhamisi wiki hii tayari kwa Tamasha la Krismasi
    03
    MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili Afrika, Rebecca Malope anatarajia kuwasili nchini kesho saa tisa alasiri kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Tamasha la Krismasi linalotarajia kufanyika keshokutwa kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

    Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama kabla ya kuwasili kwa Malope leo watawasili watangulizi wake ambao watafika kwa ajili ya kufanya maandalizi ya tamasha hilo.

    Msama alisema mwimbaji Faustine Munishi aliwasili jana usiku akitokea Kenya, ambako Sarah K anatarajia kuwasili kesho saa 10 jioni.
    Aidha Msama alisema Solomon Mukubwa anatarajia kufika Ijumaa asubuhi ambaye ataelekea moja kwa moja ukumbini kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kwa Watanzania.

    Msama alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo ili kurudisha shukrani kwa Mungu baada uchaguzi Mkuu uliofanyika kwa amani."Nawaomba Watanzania tujitokeze kwa wingi kwenye Tamasha la Krismasi ili tumrudishie Mungu shukrani baada ya kupita kwenye uchaguzi Mkuu uliofanyika kwa amani na utulivu," alisema Msama.

    Viingilio katika tamasha hilo ni shilingi 50,000 kwa Viti maalum, VIP shilingi 10,000, shilingi 5000 viti vya kawaida na shilingi 2000 kwa watoto.
    "Viingilio tulivyopanga vitasaidia wenye uhitaji maalum kama yatima, walemavu, wajane na wengineo ambao wanahitaji msaada," alisema Msama.

     Aliwataja waimbaji watakaopanda jukwaa la Tamasha la Krismasi ni pamoja na Rose Muhando, Upendo Nkone, Jesca Honore, Christopher Mwahangila, Joshua Mlelwa, Martha Mwaipaja, Christina Shusho, Sifael Mwabuka, Kwaya ya KKKT  Yombo na Kwaya ya Wakorintho wapili ambayo itazindua albamu yake ya Mchepuko sio dili.Waimbaji wa nje ni pamoja na Rebecca Malope (Afrika Kusini), Sarah K, Solomon Mukubwa na Faustin Munishi 'Malebo'  (Wote kutoka Kenya).


    Msama alisema mgeni rasmi katika tamasha hilo ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.