Jeshi la Polisi limetangaza zawadi ya Sh. milioni 20 kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Regional Cargo Services Ltd, Abdulkarid Abdi, ambaye anatuhumiwa kuwezesha kutolewa kwa makontena 329 bandarini bila ya kulipiwa ushuru.
Donge hilo nono lilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Sulemain Kova, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msako unaofanywa na polisi.
Kamishna Kova alisema Abdi ni mmoja wa wakurugenzi katika kampuni za Jas Express Freight Ltd na Ex Crearing and Fowarding Co Ltd ambazo zote zilitumika kutoa makontena hayo.
Wizi huo ulioigharimu serikali kodi ya sh. bilioni 80 ulifichuliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Dar es Salaam katikati ya mwezi uliopita.
Kova alisema baada ya kugundulika kwa 'mchezo' huo, mtuhumiwa huyo alipigiwa simu yake ya mkononi ambayo ilikuwa inaita bila kupokelewa na baadaye aliamua kuizima kabisa na kutokomea hadi sasa.
"Mtu yeyote mweye taarifa kuhusiana na mtuhumiwa huyu atoe taarifa ofisini kwangu au kwa ofisa yoyote wa polisi aliyekaribu naye au kituo chochote cha polisi kilicho karibu," alisema Kamanda Kova.
Aidha, Kamanda Kova aliwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo anatiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.
"Jeshi la Polisi linamtaka mtuhumiwa huyo ajisalimishe mapema na kwa hiari yake mwenyewe kuliko kusubiri msako mkali wa polisi, popote alipo ajue atakamatwa tu," alisema.
Kamishna Kova alisema kwenye kampuni anayofanyia kazi Abdi wanawashikiliwa watuhumiwa wengine wawili, akiwemo Mkurugenzi wa Kampuni ya Jas Express Ltd na Ofisa Forodha wa Kampuni hiyo, Godfrey Masilamba.
Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa kwa tuhuma za kuwezesha ukwepaji wa kodi ulioisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
Hata hivyo, Kova alisema uchunguzi utakapokamilika jalada la kesi hiyo litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za kisheria.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment