December 04, 2015

  • RAIS MAGUFULI AWALIPUA WAFANYABIASHARA,AWATANGAZIA KIAMA



    RAIS MAGUFULI AWALIPUA WAFANYABIASHARA,AWATANGAZIA KIAMA
    Viongozi na Wawakilishi wa Umoja wa Sekta Rais John Magufuli ametoa siku saba kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena yao kinyemela na kuyaficha kulipa kodi lasivyo yatakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
    Magufuli alitoa amri hiyo jana wakati wa mkutano wake wa kwanza na wadau  kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), jijini Dar es Salaam ambao ulijadili umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na wajibu wa Serikali kutengeneza mazingira wezeshi.
    Alisema Serikali yake itahakikisha inashirikiana na sekta binafsi ili kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha maisha ya wananchi wa chini. Aliitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji wake kwa kuangalia fursa nyingine ambazo ni muhimu katika kujenga uchumi.
    "Wale wenye makontena wasijifiche, ninatoa siku saba wakalipe kodi, tukiwakamata sheria itafuata. Nina uhakika sekta binafsi mkijipanga vizuri, tutaikomboa hii nchi," alisema Magufuli huku akishangiliwa wa wadau wa sekta binafsi.
    Alisema atahakikisha anapunguza urasimu serikalini ili mambo yote yaende kwa haraka na kuonya kuwa atakayechelewesha ulipaji wa madeni ya Serikali, atamfukuza kazi mara moja.
     "Kama mfanyabiashara yoyote atacheleweshewa malipo yake,  basi aliyechelewesha malipo hayo kama yuko chini ya mamlaka yangu ya uteuzi, hatabaki katika Serikali yangu. Huyo atakuwa anatuchelewesha tunakotaka kwenda," alisema.
    Rais Magufuli aliahidi kufuatilia mgogoro wa wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu mashine za kodi za kielektroniki (EFD) kwa kuwa hauna tija kwa taifa na kwamba suala hilo ni dogo na linaweza kutatuliwa kwa namna rahisi.
     "Muda wote wakati wanabishana, hizo pesa ambazo zingekuwa zimeingia zingetosha kununua hizo mashine. TRA ingekuwa imewapatia bure hizo mashine wakaanza kulipa kodi, ninaamini fedha hizo hazizidi Sh12 bilioni. Ni hesabu ndogo tu ambayo haihitaji elimu ya chuo kikuu," alisema
    Kwa mujibu wa Magufuli,  uchaguzi umekwisha, kila mmoja kwa nafasi yake afanye kazi ili kulikomboa taifa.
    " Tanzania imechekwa sana na nchi za jirani, sasa imefika mwisho, kila mmoja awajibike," alisisitiza Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
    Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16
     Rais Magufuli alisema hakuna fedha ya maendeleo iliyotolewa kwa wizara yoyote katika mwaka huu wa fedha wa 2015/16.
     Alisema Serikali imekuwa ikilipa mishahara  na mambo mengine ya ofisini.
    Alisema fedha hizo zimetolewa mwezi huu kiasi cha Sh120 bilioni baada ya miezi sita kupita.
    Magufuli aliongeza  kuwa hata fedha za Matumizi Mengineyo (OC),  pia zilikuwa ni tatizo hata wakati Serikali ya Awamu ya Nne."Tunapochukua hatua hizi za mabadiliko hatufanyi kwa nia mbaya ya kumkomoa mtu, bali kuwasaidia wananchi wetu. Sekta binafsi mjiamini, lakini mtangulize mbele uzalendo katika kazi zenu," alisema.
    Aliitaka sekta binafsi kushirikiana na Serikali kuboresha maisha ya wananchi.
     Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi, hivyo  hakuna haja ya kuendelea kusubiri misaada ya wahisani.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.