December 02, 2015

  • Watuhumiwa wa Kobe Wafikishwa Mahakamani


    Watuhumiwa wa Kobe Wafikishwa Mahakamani

    Wakazi watano wa Zanzibar wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya kusafirisha kobe 201 aina ya India wenye thamani ya Sh30 milioni.

    Wakili wa Serikali Ester Martin akishirikiana na Neema Mwanga, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni David Mungi (36), Mustafa Bakar (43), Mohammed Seleman (43), Salum Wakili (30) ambao ni wafanyabiashara na mvuvi, Shaban Haji (45).

    Wakili Martin alidai kuwa kati ya Novemba 1 na 16 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na Zanzibar, washtakiwa hao kwa pamoja walisafirisha nyara za Serikali kinyume cha sheria ya wanyama pori.

    Ilidaiwa kuwa Novemba 16 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), washtakiwa hao walikamatwa na kobe hao.

    Alidai kuwa washtakiwa Seleman, Wakili na Haji wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho katika maeneo tofauti walipokea na kusafirisha nyara hizo bila ya kibali cha wanyama pori.

    Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi watakapofikishwa Mahakama Kuu baada ya upelelezi kukamilika.

    Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage aliahirisha kesi hadi Desemba 14 na kuwashauri washtakiwa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.

    Washtakiwa hao walirudishwa rumande.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.