July 17, 2014

  • Ikulu: Wanaomkosoa Jakaya Kikwete Kuhusu Katiba Hawako Sahihi




    Ikulu: Wanaomkosoa Jakaya Kikwete Kuhusu Katiba Hawako Sahihi
    Ofisi ya Rais imesema kuwa wanaomkosoa Rais Jakaya Kikwete kuhusu msimamo wake katika mchakato wa Katiba Mpya hawako sahihi kwa kuwa ni mlezi na ana haki ya kutoa maoni yake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa.

    Pia, imewataka wasiokuwa wajumbe wa Bunge la Katiba waiache kazi hiyo mikononi mwa Bunge hilo kwa sasa hadi hapo rasimu itakapowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya kuikubali au kuikataa.

    Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu ikiwa ni siku moja baada ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), kutoa tamko zito kwa Rais Jakaya Kikwete ikiishangaa kauli yake ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya Watanzania.

    Rais Kikwete amekuwa akilaumiwa na taasisi na watu binafsi baada ya kulieleza Bunge la Katiba kuwa kuna baadhi ya mambo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo hayawezekani kutekelezeka, akitoa mfano wa muundo wa Muungano wa serikali tatu, jambo ambalo CCT ilisema jana kuwa alitakiwa alifanye wakati Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikimfuata kumweleza maendeleo ya kazi yao.

    Hata hivyo jana, Rweyemamu aliliambia gazeti hili kuwa: "Kinachoendelea kwa sasa kwa baadhi ya makundi ya kidini kutoa matamko dhidi ya Rais si sahihi, kwa kuwa Rais ni mlezi na ana haki ya kutoa mtazamo wake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa."

    Alisema kimsingi mchakato huo ni wa kisiasa na Rais ni mwanasiasa, pia ni mkuu wa nchi hivyo ndiye mwenye uwezo wa kutoa ushauri na kutoa angalizo pale inapohitajika, hasa anapoona kuna jambo lisilokuwa sawa, hivyo hakuna haja ya kuendelea kusimama kupinga kile alichokielekeza nje ya Bunge.

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.