Rose masaka-MAELEZO DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) imetoa ufafanuzi kuwa hajafikia muafaka wa kuwalazimisha abiria wa mikoani kutumia mchakato wa mbinu mpya ya ukatishaji wa tiketi za mabasi ya kwenda mikoani kwa njia ya mtandao ikiwemo wa simu za mkononi kwa kuwa baadhi ya wamiliki wa mabasi wamegawanyika, na bado haukidhi mahitaji ya sasa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa Mawasiliano wa SUMATRA, David Mziray wakati akizungumza na mwandishi wa habari wa Idara ya Habari(MAELEZO) baada ya Chama Cha Kutetea Abiria Tanzania(CHAKUA) kuilalamikia, SUMATRA ndio inayochelewesha mchakato huo na wameairisha kufanyika kikao cha wadau kilichotakiwa kufanyika Mei30,mwaka huu.
Malalamiko hayo yalitolewa na Mwenyekiti wa CHAKUA, Hassan Mchanjama, alipokuwa akiongea na katika mkutano na waandishi wa habari,uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).
Aidha kutokana na malalamiko hayo, Mziray alisema ni kweli kikao hicho, kiliairishwa kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika huku akisisitiza kikao hicho kilikuwa cha mashauriano na si cha kutoa uamuzi.
Mziray aliongeza kwamba , hata hivyo baadhi ya wamiliki wa mabasi hayo, wamegawanyika kwani wapo wanaouunga mkono utaratibu huo na wengine wanaupinga kutokana kwamba watakosa abiria , upatikanaji wa fedha unachukua muda mrefu na mapato yao yatajulikana.
"Hatuwezi kuulazimisha utaratibu huo utumike kwa sasa kwa sababu nilizotaja na pia kuna baadhi ya wananchi hawatumii simu za mkononi," alisema Mziray.
Mziray alisema waliishauri CHAKUA watoe elimu kwa wamiliki hao ili kuwezesha utaraibu huo utumike kwa wale wanauunga mkono na wanaoweza kuutumia, bali kwa abiria ambao ni vigumu kutumia utaratibu wa zamani utumike.
CHAKUA iimetoa malalamiko hayo kwa mamlaka hiyo baada ya kuwasilisha mchakato huo kwa kumwandikia barua , Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe , ambapo uongozi wa chama hicho ulidai kuwa aliiagiza SUMATRA kuitisha kikao na wadau .
Kikao hicho kiliitishwa Desemba 17,mwaka huu ,ambapo wadau hao ambao ni Wamiliki wa Mabasi(TABOA), CHAKUA na Jeshi la Polisi la Usalama Barabarani walikubaliana kuanzishwa kwa mchakato huo kwa kukiitisha kikao na wadau baada ya miezi mitatu.
Aidha Mchanjama amesema kuwa utaratibu waliougundua ni mzuri na wenye manufaa kwa wamiliki , abiria na Serikali kwani itarahisisha muda wa kukata tiketi bila kwenda kituo cha mabasi.
Ameongeza kwa kusema kuwa nauli zitakuwa ni halali na zilizoainishwa na SUMATRA ili kuondoa kero kwa abiria ya kuongezewa nauli hususani siku za sikukuu au shule zikifunguliwa au kufungwa.
"Utaratibu huu unarisisha abiria kudai fidia pindi anapopata madhara katika mabasi kama ajali ,kupotelewa na mzigo na magari kugoma" alisema Mchanjama.
Aliongeza kuwa kila kitu kitakuwa wazi katika mtandao, hivyo ni rahisi kwa abiria kupata nyaraka za basi husika pindi anapopata tatizo,pia mmiliki atafaidika kwa kupata mapato moja kwa moja tofauti na sasa pesa zinapita mikononi mwa watu wengi.
Kuna taasisi nyingi za serikali na watu binafsi ambazo zimekuwa mfano mzuri katika utumiaji wa mtandao ambazo ni TRA,TANESCO,DAWASCO na Benki mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment