July 17, 2014

  • Kampuni ya Precision Air Yapata Hasara ya Sh 12.1 Billion



    Kampuni ya Precision Air Yapata Hasara ya Sh 12.1 Billion
    Hali ya kifedha ya kampuni ya usafiri wa anga ya Ndege ya Precision Air bado haijatengemaa baada ya kupata hasara ya Sh12.1 bilioni katika mwaka ulioishia Machi mwaka huu. Hata hivyo, hasara hiyo ni ahueni baada ya mwaka jana kupata hasara kubwa zaidi ya Sh30.1 bilioni.

    Kwa mujibu wa taarifa ya kifedha ya kampuni hiyo ya mwaka ulioshia Machi iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari, hasara hiyo ambayo bado ni mafanikio ya ukuaji wa asilimia 60, ilichagizwa na mabadiliko ya viwango vya kubadilishia fedha, riba katika mikopo ya ndege, uchakavu wa mali na malipo mbalimbali ya kampuni.

    Hata hivyo, mafanikio hayo yanaonyesha jitihada za wazi za menejimenti kuiimarisha kampuni hiyo, ambayo mwaka jana ilijikuta ikihaha kutafuta fedha zaidi ya Sh50 bilioni ili kuongeza mtaji na ufanisi katika utoaji wa huduma zake.

    Mwaka jana, Precision iliiomba Serikali iikopeshe kiasi hicho, lakini kilishindikana baada ya ombi lao kukataliwa na hivyo kutafuta njia mbadala ikiwemo kuliomba msaada Shirika la ndege la Kenya Airways, jambo ambalo hata hivyo halijawekwa wazi utekelezaji wake.

    Moja ya mikakati iliyofanywa na Precision mwaka huo ni kuzirudisha ndege mbili zilizokuwa zikichangia hasara kwa kiasi kikubwa kwa wakodishaji wake, jambo lililosababisha idadi ya abiria wake kushuka kutoka 895, 654 wa mwaka wa awali hadi 687, 981.

    Kutokana na hatua hiyo, taarifa hiyo ilisema kiwango cha mapato kilishuka kwa asilimia 22 hadi Sh141.1 bilioni kutoka Sh181 bilioni.

    Taarifa hiyo iliyosainiwa na mwenyekiti wa Precision Air, Michael Shirima na afisa mtendaji mkuu, Sauda Rajab ilisema hata hivyo walipata faida katika kipengele cha uendeshaji kwa kupata Sh3.6 bilioni ikilinganishwa na hasara ya Sh18.1 bilioni ya mwaka ulioishia Machi, 2013 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 121.

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa mkakati wa kuiimarisha PW haukutelezwa kikamilifu hadi kipindi cha ukaguzi kilipokamilika.

    Hata hivyo, ilisema kuwa mikakati mingine kama usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha, upangaji makini wa safari na ufanisi katika uendeshaji wa safari zake, viliwezesha mapato kwa abiria yaongezeke kwa asilimia 11 ukilinganisha na mwaka uliopita. "Matumizi ya moja kwa moja yalipungua kutoka Sh147 bilioni hadi Sh99 bilioni, hali kadhalika matumizi yasiyo ya moja kwa moja yalipungua kutoka Sh44.4 bilioni hadi Sh38.9 bilioni.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.