July 25, 2014

  • Mchakato wa Ujenzi Barabara za Juu ‘flyover’ Tazara Waanza

     
     
    Tatizo la foleni katika jiji la Dar es Salaam, limeanza kupatiwa dawa baada ya Serikali ya Tanzania na Japan kutiliana saini mkataba wa ujenzi wa barabara za juu (flyover) katika makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere.

    Akizungumza baada ya kutiliana saini, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile alisema Japan imeiongezea Tanzania Sh5.64 bilioni, baada ya kiasi cha Sh52.55 bilioni kilichotolewa Juni 18, 2013 kutofikia kiwango kinachotakiwa na makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa njia hiyo ya juu.

    Sambamba na mradi huo, pia nchi hizo zimetiliana saini mkataba mwingine wa kuboresha usambazaji wa umeme katika jiji la Dar es Salaam kwa kujenga vituo vidogo katika maeneo ya Mwananyamala, Muhimbili na Jangwani Beach.

    Miradi hiyo itakayogharimu jumla ya Sh77.5 bilioni na inafadhiliwa na Serikali ya Japan, chini ya Shirika la Maendeleo la Japan (Jica).

    "Kama mnavyojua, barabara na nishati ndiyo nguzo katika ukuaji wa uchumi. Msaada huu utatuwezesha kuongeza kasi katika kuimarisha uwekezaji katika sekta ya hizi. Pia, zitachochea maendeleo katika maeneo mengine," alisema na kuongeza kuwa kiasi kingine cha Sh71.9 bilioni kimetolewa kwa ajili ya kusaidia usambazaji wa umeme jijini Dar es Salaam ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza na kukwamisha shughuli mbalimbali za uzalishaji.

    Kuhusu barabara hiyo, Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada alisema Serikali yake imeongeza fedha ili kukabiliana na upungufu wa bajeti uliosababishwa na kushuka kwa thamani ya fedha pamoja na ongezeko la bei ya vifaa vya ujenzi.

    Alisema mkataba na mkandarasi unatazamiwa kutiwa saini Septemba mwaka huu na ujenzi wa barabara hiyo utaanza muda mfupi baadaye.

    Mwakilishi Jica nchini, Yasunori Onishi alisema sekta ya usafirishaji ni moja ya shughuli kubwa wanazozifanya nchini ili kuleta maendeleo.

    Alisema shirika lake limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali ya kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam kwa miaka 30 sasa, ikiwamo ujenzi wa Daraja la Salenda ulioanza mwaka 1980. "Jica pia tulisaidia kuundwa kwa mpango mkuu wa sera na mfumo wa usafirishaji katika jiji la Dar es Salaam mwaka 2007 na 2008. Hata hivyo, katika utafiti wetu, tulipendekeza kipaumbele kielekezwe katika makutano ya Tazara," alisema Onishi.

    Alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya juu eneo hilo la Tazara, unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya watu milioni mbili wanaofanya safari zao kila siku kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwenda katikati ya jiji. Pia alisema barabara hiyo itapunguza kwa asilimia 30, muda unaotumika kusafiri katika umbali huo kutoka dakika 37 hadi dakika 25.

    "Tumejipanga kikamilifu kutekeleza maazimio tuliyosaini leo. Naiomba Serikali pia itimize wajibu wake katika kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa zinatumika katika mambo yaliyokusudiwa," alisema.

    Onishi alisema Jica ina dhamira ya dhati kuisaidia Serikali ikiwamo upanuzi wa Barabara ya Bagamoyo (Mwenge - Tegeta) ambayo ujenzi wake utakamilika mwisho wa mwezi huu.
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.