Mshtakiwa wa kwanza Rajabu Maranda anayekabiliwa na kesi ya wizi wa sh.milioni 207.2 za Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) na wenzake wanne, jana alilazimika kufika mahakamani kusikiliza kesi yake akiwa amelala kwenye kiti cha kutembelea kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya mgongo.
Mahakama ya Kisutu jana ilipanga kuendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi lakini ilishindwa kuendelea baada ya mwenyekiti wa jopo la mahakimu watatu wanaosikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru wa kikazi.
Madai hayo yalitolewa mbele ya mahakimu wawili, Ignas Kitusi na Eva Nkya, upande wa Jamhuri ulidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kuendelea na mahojiano kwa mshtakiwa wa kwanza Maranda.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Osward Tibabyekomya ambaye alidai kuwa uko tayari kuendelea na kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, Hakimu Kitusi alisema jopo linalosikiliza kesi hiyo bado halijakamilika kwa kuwa mwenyekiti wao ni mgonjwa.
Maranda kwa sasa anasumbulia na maradhi ya mgongo baada ya kufanyiwa upasuaji pamoja na shinikizo la damu na sukari hali inayomlazimu kuhudhuria mahakamani hapo kusikiliza kesi yake akiwa amelala kwenye kiti cha kutembelea.
Hakimu Kitusi alisema kesi hiyo itasikilizwa Agosti 25 na 29, mwaka huu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Farijala Hussein, Iman Mwakosya, Esther Komu na Bosco Kimela, ambao wanadaiwa kula njama ya kutenda makosa ya kughushi na kujipatia fedha.
0 comments:
Post a Comment