July 04, 2014

  • Musley Al Rawahi apania kufanya mambo makubwa Simba



    Musley Al Rawahi apania kufanya mambo makubwa Simba
    Musley Al Rawahi akisisitiza jambo.
    Mjumbe mpya wa kamati ya utendaji wa klabu ya Simba, Musley Al Rawahi, amesema kuwa silaha kubwa ya kufikia maendeleo katika klabu hiyo ni umoja na kufanya kazi kwa kujituma na uadilifu mkubwa.
    Musley ambaye mwaka jana alimzawadia gari kiungo wa Simba SC, Ramadhani "Messi" Singano kwa kucheza vizuri katika ligi kuu ya Tanzania Bara,  alisema hayo mara baada ya kutangazwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo na pia kuwa miongozi mwa wajumbe wanaounda kamati ngumu na nyeti ya usajili wa klabu hiyo.
    Alisema kuwa anashukuru kuteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji na usajili wa klabu hiyo na anaamini uteuzi wake umetokana na jinsi alivyokuwa mstari wa mbele kutafuta maendeleo ya klabu hiyo.
    Kwa mujibu wa Musley, Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva hajafanya makosa katika uteuzi wa wajumbe wa kamati ya utendaji, usajili, mashindano na soka la vijana kwani hizo ndizo nguzo za ustawi wa klabu na kufanikisha mambo mengi ya maendeleo.
    "Tukisajili wachezaji wazuri, ndiyo watatuletea ushindi ndani ya klabu na hivyo kamati ya mashindano kufanyakazi zake kwa ufanisi mkubwa, hivyo natoa wito kwa wajumbe wateule, tufanye kazi kwa bidii na kuleta maendeleo makubwa klabuni na kuendelea kumpa sifa waliotuteua kushika nadhifa hizo," alisema Musley.
    Alisema kuwa yeye ana historia kubwa sana katika klabu hiyo na amekuwa mwanachama tangu akiwa mdogo na hiyo ilitokana na mapenzi makubwa ya baba yake kwa Simba.
    "Mzee wangu amekuwa mwanachama wa klabu hii kwa miaka mingi, mimi nimefuata nyayo zake na mpaka sasa nimekuwa na klabu hii kwa miaka mingi, nina uchungu nayo sana, ninaahidi kufanya kazi kwa bidii ili kufikia lengo," alisema Musley.
    Alisema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni matarajio ya wanachama na mashabiki wa Simba kwani wanachotaka wao ni ushindi na kutwaa ubingwa.
    "Wana-Simba wanataka ubingwa, hakuna kingine ambacho wanakitaka, tunahitaji kusajili wachezaji wazuri, wenye kuleta ufanisi na kutufikisha kule tunakotaka," alisema.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.