January 29, 2015

  • Z’BAR WASHINDWA KUNUNUA NDEGE ZA VIONGOZI



    Z'BAR WASHINDWA KUNUNUA NDEGE ZA VIONGOZI
    Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kuwa haina ubavu wa kununua ndege kwa matumizi ya viongozi wake.
    Waziri wa Fedha Zanzibar, Omary Yussuf Mzee alisema hayo jana alipojibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.
    Alisema mpango huo unaweza kufanikiwa baada ya Zanzibar kuanza kuchimba nishati ya mafuta na gesi.
    Alisema SMZ itaendelea kukodi ndege kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya matumizi ya viongozi wake.
    Aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kuwa gharama za uendeshaji wa ndege za Serikali ya Muungano wa Tanzania hutolewa na Serikali ya Muungano, hivyo SMZ hulazimika kukodi na kulipia gharama.
    "Kuiweka ndege moja Zanzibar ili itumike kwa viongozi wetu wa kitaifa ni jambo linalowezekana, lakini kufanya hivyo ni kuongeza gharama za uendeshaji, kwani wakala watalazimika kuweka vifaa na wataalamu wa kuzihudumia ndege hizo," alisema Waziri Mzee.
    Awali, mwakilishi huyo alitaka kufahamu gharama za matumizi ya ndege za Serikali ikiwamo Foker 50 na 25 zinapotoa huduma SMZ kama zinalipwa na Serikali ya Muungano au wahisani.
    Pia, mwakilishi huyo alitaka kujua kwa nini ndege moja isiwe na maskani yake Zanzibar badala ya kutumika visiwani humo na Tanzania Bara.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.