January 23, 2015

  • JAMBAZI ATUPWA JELA MIAKA 45


    JAMBAZI ATUPWA JELA MIAKA 45
    Kinara wa mtandao wa ujambazi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Njile Samuel (46) maarufu John, amehukumiwa kifungo cha miaka 45 jela pamoja na kulipa faini ya Sh. milioni tatu baada ya kukiri makosa yote mawili yaliyokuwa yakimkabili.

     Mshtakiwa huyo alihukumiwa kosa la kwanza kifungo cha miaka 15 jela na faini ya Sh. milioni tatu mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Robert Oguda, baada ya kusomewa mashitaka yake.
    Ilidaiwa katika shitaka la kwanza, Januari 10, mwaka huu, saa 9:00 alasiri, eneo la Lyoma wilayani Bariadi, Njile alikamatwa na risasi 272, bunduki aina ya SMG na magazini saba.
    Katika shitaka la pili lililosomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Aidan Mwilapa, mshtakiwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 15 kwa kupatikana na bunduki, huku kosa lingine alihukumiwa kifungo kama hicho kwa kupatikana na umilikaji wa silaha bila kibali.
    Hata hivyo, adhabu hizo zitakwenda kwa pamoja na mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.
    Wiki iliyopita, Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, walikutana jijini Mwanza na kumuelezea Njile ni jambazi hatari ambaye katika kazi yake alikuwa akiwaua wenzake baada ya kufanya uhalifu.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.