Mgogoro kati ya Wakulima na Wafugaji katika bonde la Mgongola , wilayani Mvomero mkoani Morogoro umeibuka tena na kusababisha kifo cha mkulima mmoja na wengine 14 kujeruhiwa.
Waliojeruhiwa wamekatwa sehemu mbalimbli za                  miili yao na mapanga na sime za wafugaji.
            Kati ya wakulima waliojeruhiwa kwenye tukio hilo                  lilitokea jioni ya Januari 16, mwaka huu ni pamoja na                  aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ally                  Ambilikila na familia yake .
            Hata hivyo baada ya kumvamia walimpora fedha                  taslim Sh milioni tatu na kumchomea moto nyumba                  iliyokuwa ndani ya eneo la shamba lake.
            Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Leonald                  Paulo, alithibitisha kutokea kwa mapigano hayo na                  kumtaja aliyeuawa kuwa Abdallah Shomari (27) mkazi wa                  Msamvu Manispaa ya Morogoro ambaye alikuwa ndani ya                  shamba hilo na kupigwa kwa marungu na wafugaji hao.
            Kamanda Leonald amesema katika tukio hilo tayari                  jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata wafugaji wawili                  wa Kimasai ambao ni Kisaingwa Mbingwa na Rashid Saliku                  wote wakazi wa kijiji cha Kambala wilayani Mvomero.
            Alisema kwamba siku ya tukio wakulima waliamua                  kwenda kuandaa mashamba na baadaye wafugaji walienda                  katika eneo hilo na kutokea mzozo mkubwa kipindi cha                  mchana ambapo jioni yake kukatokea mapigano hayo.
            Kwa upande wa Kamanda mstaafu Ambalikila                  akielezea tukio hilo la kuvamiwa na wafugaji , alisema                  kuwa siku hiyo walienda katika bonde hilo ambalo                  wanalima tangu miaka 60 iliyopita kwa ajili ya kuanza                  kutayarisha mashamba ya mpunga kwa msimu huu.
            Alisema kuwa wakati wakiendelea kulima kwa                  kutumia trekta la kukodi ghafla lilitokea kundi kubwa la                  jamii ya wafugaji wa Kimasai wa kijiji cha Kambala na                  kuvamia eneo hilo.
            Alisema mara baada ya kuwavamia wafugaji hao                  waliwapiga kwa kutumia sime, fimbo na mapanga sehemu                  mbalimbali akiwemo yeye pamoja na familia ya watu kumi                  waliokuwa shambani kwa ajili ya matayarisho ya shamba.
            Kamanda huyo mstaafu wakati wafugaji hao                  wakiendelea kuwapiga baadhi yao walimpora fedha taslimu                  Sh milioni 3, simu na kuchoma magunia 20 ya mbegu ya                  mpunga iliyokuwa tayari kwa kupandwa katika shamba lake.
            Hata hivyo alisema baada ya tukio hilo wafugaji                  hao waliondoka na wao kupata msaada kutoka kwa wananchi                  na kuwafikisha kituo cha Polisi na baadaye kufikishwa                  Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
            Naye Said Ambilikila ambaye ni mtoto wa Kamanda                  huyo mstaafu aliyelazwa katika Hospitali ya rufaa ya                  mkoa wa Morogoro, alisema kuwa alipigwa kichwani na                  mkononi na wafugaji hao kwa kutumia silaha hizo za jadi                  baada ya kuvamiwa wakiwa katika shamba lao.
            Kwa upande wa Costa Augustino mkazi wa kijiji                  cha Dihombo wilayani Mvomero ambaye naye amelazwa                  akipatiwa matibabu kutokana na kukatwa mapanga katika                  mikono yake yote miwili na sehemu ya kichwani alisema                  baada ya kupambana na wafugaji hao alilazimika kutumia                  mbinu za kujifanya kuwa amekufa na wafugaji hao                  kuondoka.
            Alisema kuwa baada ya wafugaji hao kuona kuwa                  amekufa walitawanyika na yeye alijivuta mpaka katika                  kibanda na baadaye kuja kuokolewa na askari wa jeshi la                  Polisi waliofika eneo hilo baada ya kupata taarifa.
            Baadhi ya majeruhi wengine waliolazwa katika                  hospitali hiyo ni Rajabu Ally, Mohamed Ramadhan na                  Ramadhani Salum wote wakazi wa kata ya Kinguruwila                  manispaa ya Morogoro.
            Wakizungumza wadini hapo Mohamed Ramadhan                  alisema baada ya kupigwa aliporwa na wafugaji kiasi cha                  Sh 150,000 pamoja na simu ya mkononi, wakati Ramadhani                  Salum alidai kuporwa kiasi cha Sh 850,000 na kuchomewa                  pikipiki pamoja na nyumba yake iliyokuwa shambani kwake.
            Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa                  Morogoro,Elias Kilela, alithibitisha kupokea majeruhi                  saba waliohamishiwa katika hospitali hiyo baada ya                  kujeruhiwa na Wafugaji katika Bonde la Mgongola.
            Alisema kuwa majeruhi hao wamelazwa wadi namba                  moja hospitalini hapo huku wakiwa wamekatwakatwa na                  mapanga katika maeneo yao mbalimbali ya mwili na                  wanaendelea vizuri baada ya kuanza kupatiwa matibabu                  huku mmoja ambaye ni Kamanda mstaafu wa Polisi                  akiruhusiwa.
            Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Mkindo Patrick                  Longomeza ambaye ni miongoni mwa wakulima wanaolima                  katika bonde hilo la Mgongola alithibitisha baadhi ya                  wakulima kutoka katika kijiji chake kujeruhiwa na                  wafugaji baada kuvamiwa wakiwa katika bonde hilo.
            Alisema wakulima hao walienda katika bonde hilo                  kwa ajili ya kuandaa mashamba ya mpunga ambalo wamekuwa                  wakilima kwa muda mrefu.
            Alisema kuwa baada ya kupata taarifa walienda                  katika eneo la tukio na kuwakimbiza katika hospitali za                  Bwagara na wengine kituo cha afya cha Mvomero huku                  baadhi wakiwakimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa                  wa Morogoro ambako baadhi yao wamelazwa kwa ajili ya                  matibabu.
          
0 comments:
Post a Comment