January 06, 2015

  • KOROGWE VIJIJINI WANANCHI: TUPEWE MASHAMBA YA MKONGE TUYAENDELEZE



    KOROGWE VIJIJINI WANANCHI: TUPEWE MASHAMBA YA MKONGE TUYAENDELEZE
    Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani 'Profesa Maji Marefu'.
    Na Abdallah Juma, Tanga
    Korogwe ni moja kati ya wilaya nane zinazounda Mkoa wa Tanga. Upande wa Kaskazini, Korogwe imepakana na Wilaya ya Lushoto, Mashariki kuna Wilaya ya Muheza, Kusini kuna wilaya ya Handeni na Magharibi kuna Mkoa wa Kilimanjaro.
    Ndani ya wilaya hiyo, kuna majimbo mawili ya uchaguzi, likiwemo Korogwe Vijijini linaloongozwa na Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani 'Profesa Maji Marefu' kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
    Wiki iliyopita, Uwazi lilifunga safari mpaka kwenye jimbo hilo ambalo sehemu kubwa ipo milimani na kuzungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali ambao walieleza kero mbalimbali zilizokuwa zinawasumbua kisha akatafutwa Mbunge Maji Marefu ambaye alitoa ufafanuzi:
    Swali: Mheshimiwa Maji Marefu, Naitwa Omari Ally, tatizo letu ni kwamba bado barabara za kuunganisha kati ya Korogwe Mjini na Vijijini ni tatizo hasa kipindi cha mvua, nyingi ni za changarawe kwa nini usitujengee lami? Pia kuna Daraja la Mto Rwengela linalounganisha Vijiji vya Songea na Magoma, mvua ikinyesha kidogo tu maji yanapita juu, ni lini litafanyiwa marekebisho ili tuondokane na adha hii?
    Jibu: Wananchi wangu ni mashahidi kwa jinsi ninavyopigania jimbo letu lipate barabara za lami, bado mchakato unaendelea na tumefikia hatua nzuri. Hata hizo za changarawe, nimekuwa wakati mwingine nikitoa fedha zangu binafsi kwa kushirikiana na halmashauri kuhakikisha zinafanyiwa ukarabati mara kwa mara. Nyingi zinapitika misimu yote na hizo chache nazo tunazishughulikia kwa ukamilifu.
    Swali: Naitwa Maimuna Ally, mkazi wa Kijiji cha Kwetonge. Adha kubwa hapa kijijini kwetu, hatuna maji ya bomba tunatumia maji ya mito na visima vya wazi ambayo ni hatari kwa afya zetu na familia zetu. Ni lini na sisi tutapatiwa huduma ya maji ya bomba kama vijiji vingine?
    Jibu: Maeneo mengi tayari yanapata huduma ya maji ya bomba na kwa vijiji vichache ambavyo bado, nawaomba wananchi muwe na subira kwani hii miradi inatekelezwa kulingana na bajeti ya serikali. Pia maeneo mengine tunaendelea kuchimba visima.
    Swali: Mheshimiwa mbunge, sisi wananchi wa Korogwe Vijijini tunaomba tupatiwe ardhi kwenye mashamba ya mkonge kwani mengi yametelekezwa na wawekezaji na sisi wananchi hatuna sehemu za kulima, kwa mfano shamba la Kerenge Mremwa ambalo halifanyi kazi kabisa, tunaomba tugawiwe wananchi.
    Jibu: Mashamba yote ya mkonge ambayo hayazalishi, tunafikiria kuwapa wananchi ili wayatumia kwa uzalishaji wa mazao mengine wakati jitihada za kufufua zao la mkonge zikiendelea. Wananchi wote wanaoishi jirani na mashamba, watanufaika baada ya mchakato kukamilika.
    Swali: Mheshimiwa mbunge, naitwa James Zayumba. Sisi wananchi wa Mombo, Bungu na Magoma kero yetu kubwa ni katika sekta ya afya. Hospitali ya Mombo na vituo vya afya vya Bungu na Magoma, kuna wakati ukienda kwa ajili ya matibabu unaambiwa hakuna dawa tukanunue wenyewe. Je, ni lini hilo tatizo litaondoka?
    Jibu: Ni kweli kuna tatizo la upungufu wa dawa kwenye hospitali na vituo vya afya na hili ni tatizo la nchi nzima. Kwa kushirikiana na serikali na wafadhili, tunaendelea kulishughulikia na naamini kero hiyo itaisha kabisa.
    Matatizo mengine yaliyoainishwa na wananchi wa jimbo hilo, ni uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi na uwindaji haramu katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambapo mbunge huyo amekiri kuyafahamu na kueleza hatua mbalimbali ambazo anaendelea kuzichukua kwa kushirikiana na serikali kuu.
    Wiki kadhaa zilizopita, Gazeti hili lilichapisha kero za wananchi wa Jimbo la Temeke lakini mbunge wa jimbo hilo, Abbas Mtemvu hakuweza kupatikana kuzijibu. Jitihada za kumtafuta zinaendelea na atakapopatikana, atatoa majibu kupitia ukurasa huu- Mhariri.
    Je, umeridhishwa na majibu ya mbunge wako? Tuma ujumbe mfupi wa maandishi kwenda namba 0782-398 690 au barua pepe kwa anuani ya uwazinewspaper@yahoo.com


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.