January 25, 2015

  • UKOSEFU WA AJIRA NCHINI NINI SULUHISHO LAKE?



    UKOSEFU WA AJIRA NCHINI NINI SULUHISHO LAKE?
    Mara kadhaa, watu wa kada mbalimbali wakizungumzia tatizo la ajira nchini, baadhi ya viongozi wa serikali huwakejeli na kudai kuwa hawana hoja za msingi.

    Viongozi hao wamekuwa wakieleza mikakati ya Serikali kuhusu kuwapatia Watanzania ajira, mipango ambayo kwa kiasi kikuwa ipo katika makaratasi tu lakini kwa uhalisia hali ni mbaya.
    Nikupe mfano wa mwaka 2006. Utafiti uliofanyika mwaka huo unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 12 ya vijana nchini hawana ajira na wengi wa vijana hao wako mijini, yaani asilimia 15 tu ya vijana milioni 25 ndio wenye ajira.
    Asilimia 70 ya vijana wenye miaka kati ya 13 na 34 ambao ni wengi zaidi kati ya idadi ya watu milioni 45 waliopo Tanzania ni kundi kubwa ambalo ni tegemezi na halina ajira na hii ni kati ya nguvu kazi ya vijana milioni mbili na nusu ambao wako mijini na hawana ajira.
    Vijana zaidi ya 850,000 wanahitimu masomo kila mwaka huku wakiwa tayari kuingia kwenye soko la ajira lakini inasikitisha kati ya hao, ni asilimia 5 ndio wanaopata ajira ya kudumu na asilimia 35 ikijikita katika kilimo ambacho bado kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo zile za uhaba wa pembejeo.
    Hivi sasa vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali na wengi wakiishia mitaani kutokana na kukosa ajira.
    Hao 30,000 ni wale ambao walifanikiwa kupenya darasa la saba, kidato cha nne na sita. Maana yake ni kwamba wapo vijana wengi walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali.
    Wapo walioishia darasa la saba na kuingia mtaani na wapo walioishia kidato cha nne na sita na kuishia hukohuko mitaani, huku wakiwa hawana ujuzi wowote.
    Tatizo la ajira nchini kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya mfumo mbovu wa elimu ambao unazaa vijana wengi wasio na uwezo wa kuajiriwa popote na hata kujiajiri.
    Elimu bora inayokidhi mahitaji ya taifa ndio njia mojawapo na mwafaka ya kutatua tatizo la ajira nchini kwani fursa za ajira zimejaa duniani kote na wanaozifaidi ni wale wenye maarifa na ujuzi ambao msingi wake mkuu unatokana na elimu bora wanayoipata.
    Mfano, nchi yetu haina vyuo vya ufundi vya kutosha ambavyo vitaweza kuwapokea vijana walioshindwa kuendelea na sekondari kutokana na sababu mbalimbali.
    Ni kazi rahisi, kuanzisha vyuo vya ufundi nchi nzima gharama yake ni takriban Sh800 bilioni.
    Kama fedha hiyo ni nyingi unaweza kuwekwa utaratibu katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ikatolewa elimu ya ufundi na baada ya mafunzo vijana wapewe vitendea kazi kupitia mikopo kutoka mifuko ya hifadhi za jamii na kutakiwa kurejesha baada ya kuanza kuzalisha fedha kupitia shughuli watakazoanza kuzifanya.
    Kwa sasa hali ni mbaya kwasababu hata wanaomaliza vyuo vikuu wanakosa maarifa na asilimia kubwa husubiri kuajiriwa katika nchi ambayo kwa mwaka inatengeneza ajira kwa kiasi kidogo sana.
    Achilia mbali elimu, nchi imelala katika sekta ya viwanda wakati sekta hiyo ndio inayoweza kuajiri watu wa aina yoyote, wenye ujuzi na wasio na ujuzi, wenye elimu na wasio na elimu,
    Kuimarisha sekta ya viwanda maana yake ni kuinua sekta ya kilimo ambayo ni eneo muhimu la kutatua tatizo la ajira. Kwa kujenga uchumi wa viwanda maana yake utahitaji malighafi ambazo zinazalishwa hapa nchini.
    Kujenga viwanda vya kubangua korosho maana yake unawahamasisha wananchi wa mikoa ya kusini mwa Tanzania kulima kwa wingi korosho maana unawahakikishia soko la korosho zao.
    Kujenga viwanda vya kusindika matunda maana yake unawahamasisha wananchi walime kwa wingi matunda kwa kuwa unawahakikishishia soko la matunda yao.
    Pia, kujenga viwanda vya nguo maana yake unawahamasisha wananchi walime kwawingi pamba kwa kuwa unawahakikishia soko la pamba yao.
    Matokeo yake vijana wanaodunduliza 'visenti' vyao kufungua biashara zao kandokando ya barabara kwa lengo la kujipatia riziki, wanafukuzwa na mabomu ya machozi bila kupewa au kupelekwa maeneo mbadala watakayoweza kufanyia biashara zao.
    Wakati mwingine wakipelekwa katika maeneo, aidha yatakuwa hayana miundombinu au yatakuwa mbali na makazi ya watu.
    Kama serikali haitaki haya iwekeze kwenye elimu, ijenge uchumi wa viwanda, ifanye mapinduzi ya kilimo kwani ndio suluhisho la kudumu la tatizo la ajira nchini.
    Najua kuwa kuna mikakati ya utekelezaji wa mipango mbalimbali yenye lengo la kukuza ajira ambayo ni mpango wa mafunzo yenye kuwezesha vijana kujiajiri, mfuko wa maendeleo ya vijana, mpango wa kukuza ajira kwa vijana na mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kukuza ajira.
    Sawa, ila kinacholalamikiwa na wengi ni kushamiri kwa mipango ya kwenye makaratasi, mipango ambayo hata ukiambiwa imetekelezwa haiendani na hali halisi ya maisha ya Watanzania.
    MWANANCHI.



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.