January 02, 2015

  • EWURA: MAFUTA KUSHUKA MWANZONI MWA MWEZI FEBRUARI..PIPA LILIKUWA LINAUZWA DOLA 110 SASA LINAUZWA DOLA 60


    EWURA: MAFUTA KUSHUKA MWANZONI MWA MWEZI FEBRUARI..PIPA LILIKUWA LINAUZWA DOLA 110 SASA LINAUZWA DOLA 60

    Kushuka kwa bei. Ni mara ya kwanza tangu 2009 bei ya mafuta katika soko la dunia imeshuka kwa asilimia 50 tofauti na miaka ya nyuma.Meneja Mkuu PIC, Michaele Minja anasema iwapo itaendelea kuwa hivi hivi, huenda bei ikashuka zaidi.  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imesema bei ya mafuta nchini inaweza kushuka kwa kiwango kikubwa ifikapo mwanzoni mwa mwezi Februari.Meneja uhusiano na mawasiliano wa mamlaka hiyo, Titus Kaguo alisema jana kuwa hilo linatokana na thamani ya shilingi kuporomoka dhidi ya Dola ya Marekani na pia muda ambao mafuta yanayouzwa sasa nchini, yalinunuliwa.Bei ya mafuta duniani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009, imeshuka kwa zaidi ya asilimia 50.
    Dunia imeshuhudia tangu Juni mwaka jana, bei ya nishati hiyo ikishuka kutoka Dola 110 ya Marekani mpaka Dola 60 kwa pipa moja la mafuta ghafi, hali inayoelezewa kuwa ingezisadia nchi zisizozalisha nishati hiyo.
    Lakini Kaguo alisema hilo halitaweza kuonekana kwa sasa hadi mwanzoni mwa Februari.
    "Bei imeshuka kwenye soko la dunia lakini thamani ya shilingi yetu inaendelea kuanguka kila siku, hii inasababisha kutoonekana kwa tofauti hapa nchini kwa kuwa bado tunaagiza bidhaa hiyo kwa Dola ya Marekani," alisema.
    Hata hivyo, Kaguo alisema kumekuwa na unafuu wa bei ya nishati hiyo katika miezi kadhaa iliyopita.
    "Bei inaweza ikawa nzuri zaidi kuanzia mwishoni mwa Februari kwa kuwa mafuta yanayoagizwa sasa ndiyo yatakuwa yameingia sokoni, lakini muhimu zaidi ni kuimarika kwa shilingi yetu dhidi ya Dola ya Marekani," alisema.
    Takwimu za Ewura zinaonyesha bei ya mafuta imekuwa ikipungua katika miezi miwili mfululizo.
    Mpaka Desemba 3, bei ya petroli ilikuwa imepungua kwa Sh149 kwa lita wakati dizeli ilipungua kwa Sh119 huku mafuta ya taa yakishuka kwa Sh106 kwa lita ikilinganishwa na Novemba.
    Meneja mkuu wa usimamizi wa uagizaji wa mafuta wa pamoja (PIC), Michael Mjinja alisema mwagizaji anayeleta mafuta kwa sasa alishinda zabuni hiyo mwezi Oktoba mwaka jana.
    "Kwa hiyo mafuta yaliingizwa tangu Novemba yakaanza kutumiwa Desemba," alisema.
    Alisema kampuni iliyoagiza mafuta yatakayotumika Februari, alishinda zabuni hiyo Desemba, 2014.
    "Mafuta yatakayoagizwa kwa ajili ya matumizi ya Februari, yananunuliwa kwa bei ya sasa kwenye soko la dunia lakini yatauzwa Februari," alisema.
    Alisema hata kama katika kipindi hicho mafuta yatapanda au kushuka, bei elekezi itakuwa ni ile ile iliyofungwa wakati wa utoaji wa zabuni.
    "Kama bei ya mafuta kwenye soko la dunia itaendelea kushuka ni matarajio yetu kwamba hapa nchini pia itaendelea kushuka," alisema.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.