January 14, 2015

  • WATANZANI 10 000 KUAJIRIWA NA DANGOTE



    WATANZANI 10 000 KUAJIRIWA NA DANGOTE
    BILIONEA namba moja Afrika anayemiliki mtandao wa viwanda vya saruji Afrika, Alhaji Aliko Dangote anatarajia kuajiri zaidi ya watu 10,000 katika kiwanda chake cha kisasa, kinachojengwa kwa kasi eneo la Msijute, Mtwara kinachotarajiwa kuanza kazi Agosti mwaka huu.


    Aidha, amepania kubadilisha miundombinu kadhaa ya mji wa Mtwara, akilenga kujenga soko la kisasa, hospitali kubwa, shule na kituo kikubwa na cha kisasa cha Polisi kitakachojengwa katika eneo la ekari sita.
    Hayo yalisemwa na Mwakilishi Mkazi wa kampuni ya Dangote nchini, Esther Baruti- Kroll, wakati alipokuwa anatoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho, kinachotarajiwa kuwa kikubwa zaidi Afrika Mashariki, mbele ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) kiwandani hapo.
    Alisema kiwanda kitakapoanza kazi, kitaajiri watu 10,000, kati yao 1,000 ni wale watakaoajiriwa moja kwa moja kiwandani.
    "Kwa kweli ujio wa kiwanda hiki ni ukombozi kiuchumi na pia kitasaidia vijana kupata ajira, hivyo kuisaidia serikali katika harakati za kuhakikisha inaondoa tatizo la ajira kwa vijana…tutaajiri zaidi ya watu 10,000," alisema mwakilishi huyo aliyesisitiza kuwa, nafasi za kazi zitaanza kutangazwa hivi karibuni.
    Alisisitiza: "Sisi hatujatangaza nafasi za kazi, ila tutafanya hivyo hivi karibuni. Watu wasihangaike na wengine wanaotumia mitandao ya kijamii kupotosha umma juu ya ajira za Dangote. Wajiandae kufuata utaratibu sahihi utaokaotangazwa nasi kupitia magazeti ya Daily News na HabariLeo."
    Huduma za kijamii
    Aidha, alisema pamoja na ajira, kampuni ya Dangote inakusudia kuboresha huduma za kijamii kwa kujenga soko kubwa na la kisasa mkoani Mtwara, hospitali ya kisasa, shule la kituo cha kisasa cha Polisi mkoani Mtwara, akisema eneo la ekari sita limetengwa kwa ajili ya kituo cha Polisi.
    Kwa upande wa wananchi mmoja mmoja, alisema kampuni ya Dangote inatarajia kuanzia mwezi ujao kukopesha fedha kiasi cha Sh milioni 450 kwa wakazi wa vijiji kumi vinavyozunguka eneo la mradi.
    "Alhaji Aliko Dangote aliahidi kusaidia wakazi wa maeneo jirani, akaahidi kwa kuanzia angetoa Sh milioni 450 kupitia kwenye vikundi. Tumeshajiridhisha, watu wamejiunga hivyo fedha zitaanza kutolewa mwezi ujao (Februari) ili watu wawe na shughuli za kufanya…" alisema Baruti.
    Kujenga bandari
    Mbali ya kukusudia kuzalisha umeme wake kama uongozi wa kiwanda hicho ulivyoomba kibali cha kufua umeme wake wa megawati 75 kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Umeme (Ewura) kwa ajili ya kiwanda na wakazi wanaozunguka eneo hilo, kampuni ya Dangote pia inakusudia kujenga bandari yake mjini Mtwara.
    Mwakilishi wake alisema itajenga bandari umbali wa kilomita 20 kutoka kiwandani lengo likiwa kurahisisha usafirishaji wa saruji yake itakayozalishwa kwa wingi zaidi kuliko kiwanda kingine chochote katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
    Mbali ya bandari, alisema wanatarajia kuingiza nchini malori 600 kwa ajili ya kuhakikisha saruji inafika kila kona ya Tanzania ili kurahisha upatikanaji na pia kumpunguzia mteja gharama za kufuata mbali bidhaa hiyo.
    "Tunataka kumfikia kila Mtanzania ili awe na nyumba ya kisasa kwa gharama zisizo kandamizi… tutauza pia nje ya nchi kwa sababu saruji tutakayozalisha ni nyingi sana, zaidi ya tani 7,500 kwa siku," alisema Baruti. Alisema kwa kiasi kikubwa saruji itasafirishwa hadi Dar es Salaam kwa meli na baadaye kusambazwa ndani na nje ya nchi.
    Kwa sasa, gharama ya saruji iko juu huku usafiri ukitajwa kuwa chanzo cha ongezeko hususani kwa mikoa ya pembezoni. Wakati jijini Dar es Salaam, bei yake ni kati ya Sh 13,000 na 15,000 kwa mfuko wa kilo 50, baadhi ya mikoa, bei inazidi Sh 20,000.
    Pamoja na madai ya usafiri kuchangia gharama za saruji, bei hiyo ya juu pia imechangiwa na uwezo mdogo wa viwanda vinne vya ndani, ambavyo vimeshindwa kukidhi mahitaji.
    Kwa sasa mahitaji ya saruji nchini ni tani milioni tatu kwa mwaka, wakati viwanda vilivyopo vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.2. Kiwanda cha Dangote nchini katika hilo, kimepanga kuzalisha tani milioni 3 na kuuza katika soko la ndani na nje.
    Dangote anayeongoza kwa utajiri barani Afrika huku akishika nafasi ya 23 duniani, anamiliki utitiri wa biashara na kwa upande wa saruji, ana viwanda 16 barani Afrika.

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.