January 06, 2015

  • WAKATI TUNAINGIA 2015, TUJIKUMBUSHE MIKATABA MIBOVU ILIYOIGHARIMU NCHI


    WAKATI TUNAINGIA 2015, TUJIKUMBUSHE MIKATABA MIBOVU ILIYOIGHARIMU NCHI
    Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Mhongo.
    MUNGU ni mwema na ndiyo maana leo wasomaji wa safu hii mnaisoma huku mkiwa na afya njema. Tumhimidi Mungu aliyetuumba milele, amina.
    Baada ya kusema hayo niseme machache kuhusu mikataba mibovu ambayo imeiingizia taifa hili hasara kubwa ambayo taifa linahujumiwa.
    Mikataba hii inanifanya nijiulize, baadhi ya watu, Watanzania wanasoma na kupewa nyadhifa za kufanya kazi kwa niaba ya nchi walisoma ili kuiangamiza nchi au kuitetea isizame?
    Kati ya mwaka 1995 na 2007, nchi yetu ilighubikwa na mikataba ya uwekezaji ya kifedhuli, iliyosababisha mabilioni ya fedha kukwapuliwa na mafisadi wa ndani na nje ya nchi na kufichwa katika mabenki ya ughaibuni.
    Baadhi ya mikataba hiyo hatari ya uwekezaji, ni pamoja na ule wa mradi wa Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na serikali, kupitia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco).
    Chini ya mkataba huo wa miaka 20, nchi imeporwa mabilioni ya fedha na inaendelea kuchunwa na kutupwa gizani kwa kukosa umeme, ingawa itaendelea kuilipa IPTL zaidi ya shilingi bilioni 5.0 kwa mwezi kwa umeme usiokuwepo, kuanzia mwaka 1999 hadi 2019.
    Walioiingiza nchi katika kashfa hiyo wanafahamika kwa majina, lakini wamekumbatiwa na kutakaswa ili watakasike na baadhi ya watu wasiokuwa na uchungu wa nchi hii wanawaona ni wajanja!
    Kashfa nyingine zenye kuhusisha mabilioni ya fedha, ni pamoja na ile ya EPA (ilihusisha shilingi bilioni 133), ununuzi wa rada na ndege mbovu ya rais kwa kile kilichoelezwa na Waziri wa Fedha wa wakati huo, Basil Mramba kwamba rais hawezi kupanda punda kama Yesu wa Nazareth. Ndege hiyo mbovu ilinunuliwa shilingi bilioni 40.
    Nyingine ni ubinafsishaji wa Benki ya NBC na uuzaji wa nyumba za serikali kwa bei ya kutupa, pamoja na kuuzwa kwa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira, bila kusahau sakata la mradi wa umeme wa kitapeli wa Richmond/Dowans; Loliondo, ufujaji wa shilingi bilioni 150 za Mfuko wa Uagizaji Bidhaa Nje (CIS) na mikataba mibovu ya madini, kwa kutaja michache tu.
    Haya yametokea na hakika wasomi wote waliohusika na hujuma hii wanapaswa kulaaniwa na wananchi wote wazalendo wa nchi hii.
    Serikali imejitahidi kuficha ukweli wa kashfa hizi lakini Mungu amewapenda zaidi wananchi na haya mambo yakajulikana. Kashfa moja kabambe, inayohusu Mradi wa Mgodi wa Meremeta ililipuliwa bungeni na  ilifikia Bunge kuitaka serikali iwasilishe hesabu za kampuni hiyo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ziweze kukaguliwa ili kukata mzizi wa fitina.
    Tunaipa umuhimu wa pekee kashfa hii ya Meremeta kwa sababu ni kielelezo cha wazi kwa serikali kuhusishwa moja kwa moja katika uporaji wa rasilimali za taifa na kugeuka mbogo kuwahadaa wananchi baada ya kugunduliwa kwa kisingizio cha fedha zilizoporwa kutumikia usalama wa nchi.X
    Katika kashfa hiyo,  zaidi ya shilingi bilioni 155 zililipwa kutoka Benki Kuu (BoT) kwenda Benki ya NedBank ya Afrika Kusini kama malipo ya mkopo uliodhaminiwa na serikali kwa mradi huo wa uchimbaji dhahabu.
    Serikali ilibanwa na Bunge na kuagiza mahesabu yakaguliwe, haikutii na aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG) Ludovick Utouh, alinukuliwa baadaye akilalama: "Nitakagua nini wakati sijapata hesabu zenyewe kutoka serikalini…?
    Kampuni ya Meremeta, ambayo baada ya mambo kufichuka ilibadilishwa jina kiujanjaujanja na kuitwa Tangold.
    Wabunge walikatazwa kuijadili kwa sababu za kiusalama. Je, kuna ukweli gani kwamba Kampuni ya Meremeta haizungumziki kwa sababu inagusa Usalama wa Taifa? Je; ni kampuni ya serikali? Malipo hayo na mengine ndiyo yaliyozua utata na Bunge kuagiza hesabu zikaguliwe.
    Napenda kutaja wazi hapa kwamba Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwa namna yoyote ile, haihusiki na sakata zote hizi, ingawa inazijua fika, hivyo,  imejitahidi kuziatamia bila mafanikio kwa njia ya kufunika kombe mwanaharamu apite na mambo kama hayo yamemgharimu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredirick Werema.
    Serikali ifahamu kwamba kwa misingi ya sheria, kitendo cha mtu kufunika kosa lililotendwa na mtu mwingine, kwa lengo la kumwepusha sheria isichukue mkondo wake, kinamfanya mtu huyo mwenye kutaka kumwokoa mwingine kuwa mshiriki wa kosa hilo kwa kiwango sawa na cha mtuhumiwa halisi wa kosa.
    Kwa hiyo, viongozi wanaowalinda au kuwasafisha mafisadi wana hatia ya ufisadi uleule wa wale wanaowaokoa.
    Nia ya kukumbushana ufisadi huu ni kuwataka wanaokabidhiwa dhamana ya kulinda rasilimali za nchi hii kuwa na uzalendo  wa kweli na kuachana na rushwa au hujuma kwa taifa.
    Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.