Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendana na kasi ya Mpango wa MATOKEO Makubwa Sasa (BRN) katika utendaji wao hasa katika eneo la ufuatiliaji na uadilifu.
Waziri Mkuu Pinda ameyasema hayo leo (Jumatano) mjini hapa wakati wa hotuba yake fupi ya ufunguzi wa Mkutano wa siku tatu wa watendaji hao kujitathmini katika utekelezaji wa miradi ikiwemo miradi ya elimu iliyoko chini ya BRN. Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
BRN ni Mpango ulioasisiwa na Serikali ya Tanzania na kuanza kazi Julai mosi, 2013 ukiwa na malengo ya kuleta mfumo mpya wa kuweka vipaumbele, kutekeleza miradi kwa wakati na watendaji kuacha kufanyakazi kwa mazoea.
Sekta sita za awali zilizoingizwa katika vipaumbele vya BRN ni elimu, maji, kilimo, nishati, uchukuzi na ukusanyaji wa mapato. Sekta za uboreshaji wa mazingira ya biashara na afya ziko mbioni kuingia katika BRN. Utekelezaji wa BRN unasimamiwa na Kitengo kipya cha Rais cha Usimamizi wa Miradi (PDB).
Bw. Pinda alitumia muda huo kusisitizia kuwa BRN imeleta kasi nzuri katika utekelezaji wa miradi kwa kusisitizia uwajibikaji na malengo. Aliwahamaisha viongozi hao kushirikiana na wataalamu mbali mbali wanaofanya kazi zao katika maeneo ya mikoa na wilaya ili kufanikisha maendeleo ya Taifa.
Akifafanua zaidi utendaji kazi chini ya BRN, Waziri Mkuu alisema Mpango huo unawalazimu watendaji hao kuwajibika ipasavyo katika ushirikishaji, usimamizi makini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbali mbali ya Serikari.
Alitumia pia fursa hiyo kuwataka viongozi hao waandamizi kuhakikisha kuwa katika utekeleaji huo wa miradi unakuwepo ushirikiano na wakandarasi wenye sifa kwani ubadhirifu na upendeleo katika utoaji wa miradi umekuwa ukirudisha nyuma maendeleo na kuwakwaza wananchi.
Kwa upande wake Mratibu wa Masuala ya Utawala Serikalini kutoka Ikulu, Francis Mang'ila siri ya nchi kupata maendeleo ni kwa watendaji wote ngazi za mikoa na wilaya, kutatua malalamiko mbali mbali yanayowafikia kwa kuzingatia wakati badala ya kuacha wananchi wakilalamika.
Alisema hali iliyopo sasa inapaswa kubadilika ambapo badala ya wananchi kuwasilisha zaidi matarajio wamekuwa wakiwasilisha malalamiko kutokana na watendaji waandamizi wa mikoa na wilaya kushindwa kufanyiakazi kero zao mapema.
0 comments:
Post a Comment