August 02, 2014

  • Watuhumiwa wa mabomu wapandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya mauaji




    Watuhumiwa wa mabomu wapandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya mauaji
    Watuhumiwa wapatao 19 wanaotuhumiwa kwa milipuko ya mabomu mkoani Arusha leo wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha na kusiomewa mashtaka mbalimbali yanayo wakabili yakiwemo ya mauaji.Watuhumiwa hao ambao wameunganishwa na wenzao zaidi ya 20 waliokwishafikishwa kwenye mahakama hiyo kwa tuhuma hizo wamefikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi ambao haujawahi kuonekana katika siku za hivi karibuni.


    Gari ya polisi iliyowabeba watuhumiwa hao 

     Tofauti na ilivyokuwa hapo awali ulinzi katika mahakama hiyo uliiimarishwa kwa kiasi kikubwa kuanzia mapema alifajiri ambapo watu wote waliokuwa wanaingia kwenye lango la mahakama hiyo walikaguliwa na vifaa maalumu utaratibu ambao ulifuatwa na watu wote bila kujali nyadhifa zao wakiwemo watendaji wa mahakama hiyo.

    Baada ya kufikishwa mahakamani hapo mbele ya hakimu Devota Msofe aliyekuwa anasaidiwa na waendeshamashtaka Agustino Kombe, Felexs Kwetukia na Maselina Mwamunyange washtakiwa walisomewa mashtaka yanayowakabili kwa makundi, jinsi wanavyodaiwa kuhusika na madhara yaliyosababishwa na makosa hayo.


    Miongoni mwa mashataka waliyosomewa ambayo kila mmoja alihusishwa kwa namna moja ama nyingine huku baadhi yao wakijikuta wakitajwa karibu kwenye makosa yote ni pamoja na shtaka la mauaji, kujihusisha na vitendo vya kigaidi, kukusanya silaha yakiwemo mabomu, kuyasarisha na kisha kuyatumia kuua na pia kufadhili vitendo hivyo kwa kutoa fedha na ushirikiano wa kuvitelekeza.

    Mashtaka mengine ni pamoja na kushawishi na kuhamasisha vijana kujiunga na vikundi vya ugaidi, kuhifadhi dhana na silaha za kwa lengo la kufanya ugaidi na kuzitumia kutekeleza vitendo hivyo.

    Kesi ya watuhumiwa hao ambao wote wanahusishwa na matukio yote ya milipuko ya mabomu na kuwamwagia viongozi wa dini tindikali vilivyowahi kutokea mkoani Arusha itatajwa tena tarehe 15.08/2014 na washtakiwa wote wamerudishwa rumande ambapo kwa mujibu wa sheria kesi yao haina dhamana.



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.