March 14, 2016

  • MKAPA ANVYOKUBALIKA KUREJESHA AMANI BURUNDI



    MKAPA ANVYOKUBALIKA KUREJESHA AMANI BURUNDI  Rais mstaafu wa Tanzania,          Benjamin Mkapa
    Bujumbura, Burundi. Burundi imeunga mkono kuteuliwa mpatanishi mpya kwa ajili ya kujaribu kutatua mgogoro wa nchi hiyo ambao umesababisha mamia ya raia kufa huku wengine wakikimbilia nchi jirani na kuishi kwenye kambi za wakimbizi.



    Chama tawala cha CNDD-FDD kimesema kuwa kuteuliwa kwa rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa kuwa mpatanishi mpya wa nchi hiyo ni hatua nzuri katika kuharakisha juhudi za kutatua mgogoro unaoendelea kufukuta.

    Mwenyekiti wa chama hicho, Pascal Nyabenda amesema Mkapa ana wakati mwingi wa kuzungumza na makundi yote nchini humo na wananchi ili kuandaa mazingira ya kufikiwa matokeo mazuri ya kurejeshwa amani na utulivu.
    Kiongozi huyo wa Burundi amesema kuwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ataendelea kusalia katika nafasi yake ya kusaidia kuboresha mazingira ya mazungumzo ya Burundi, lakini yeye peke yake hawezi kusimamia mazungumzo hayo.
    Katika kikao chao cha hivi karibuni viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliokutana mjini Arusha walimteua Mkapa kuwa mwenyekiti wa kundi la upatanishi wa mgogoro wa Burundi.
    Awali, Rais Museveni alikuwa ameteuliwa kuwa mpatanishi wa mgogoro huo. Licha ya kufanya vikao kadhaa vya mazungumzo na viongozi wa Burundi, hakufanikiwa kupata matokeo yoyote ya kuridhisha.
    Baadhi ya wataalamu wa mambo walikosoa kuchaguliwa Rais Museveni kuwa mpatanishi wa mgogoro huo na hivyo tokea mwanzoni walikuwa wametabiri kufeli upatanishi wake.
    Wiki iliyo iliyopita, marais wa nchi tano za Afrika za Mauritania, Uganda, Senegal, Gabon na Waziri Mkuu wa Ethiopia wakiongozwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini waliitembelea Burundi na kutaka mazungumzo ya haraka yafanyike ili kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
    Hivi sasa kukubaliwa mpatanishi mpya wa mgogoro wa Burundi na viongozi wa Serikali ya nchi hiyo ni ishara nzuri kuwa viongozi hao wako tayari kuchukua hatua ya kutatuliwa kwa amani mgogoro huo ambao ulianza miezi kumi iliyopita kutokana na uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena urais kwa mara ya tatu mfululizo.
    Wengi wanaieleza hatua hiyo ya Rais Nkurunziza ni kwenda kinyume na katiba ya nchi na mazungumzo ya amani ya Arusha Tanzania.
    Mivutano ya kisiasa na ghasia za ndani zimefikia hatua ambayo inaoonekana na wa juzi wa mambo kuwa zinaweza kuanzisha tena vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
    Kutokana na ukweli huo, ndipo jamii ya kimataifa na hasa Umoja wa Afrika (AU) ukaanzisha juhudi kubwa katika siku za hivi karibuni kwa madhumuni ya kutatua kwa amani mgogoro wa nchi hiyo.
    Viongozi wa umoja huo wanasema kuwa vita vya aina hiyo huko Burundi vinaweza kuhatarisha usalama wa nchi nyingine za eneo hilo, na ndiyo maana wakasema kuwa hawataruhusu vita hivyo kutokea. Wanamatumaini kuwa mgogoro huo unaoendelea utapatiwa ufumbuzi.
    Hata kama mazungumzo ya kutatua mgogoro wa Burundi hayajafanikiwa, lakini kufuatia safari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon na kisha ya viongozi kadhaa wa nchi za Afrika nchini humo, inaonekana kuwa mapatano ya kuhitimishwa mgogoro huo yamefikiwa kwa kiwango fulani.
    Matumaini hayo yanapata nguvu zaidi hasa baada ya Burundi kukubali kutumwa nchini humo waangalizi wa kijeshi 100 wa Umoja wa Afrika.
    Vilevile, imekubali waangalizi 100 wa haki za binadamu.
    Awali, Rais Nkurunziza alikuwa amedai kuwa kutumwa nchini kwake waangalizi hao ni uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi hiyo.
    Wiki iliyopita mkuu wa chama cha upinzani cha Front for Democracy in Burundi, Ngendakumana, LĂ©once alisema baada ya kukutana na ujumbe wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika wamekubaliana kuimarishwa upatanishi wa mgogoro wa nchi hiyo.
    Mgogoro huo hadi sasa umesababisha mamia ya watu kuuawa, kujeruhiwa na maelfu ya wengine kugeuka wakimbizi.
    Kutokana na juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kumaliza mgogoro huo, watu wa Burundi na jamii ya kimataifa wana matumaini kwamba mazungumzo ya amani yataanza hivi karibuni kwa shabaha ya kuhitimisha mgogoro huo wa kisiasa, ivyo kurejesha tena nchini humo usalama, amani na utulivu wa kudumu.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.