March 06, 2016

  • WANAWAKE WAHIMIZWA KUSHIRIKI KWENYE MICHEZO



    WANAWAKE WAHIMIZWA KUSHIRIKI KWENYE MICHEZO
    jen3
    Na Fatma Salum  (MAELEZO) 
    Wanawake nchini wamehimizwa kushiriki kwenye michezo mbalimbali kuanzia ngazi ya vijiji hadi taifa ili kuboresha afya zao na kujiongezea kipato.
    Hayo yamesemwa na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Kazi Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama leo jijini Dar es Salaam wakati akihutubia kwenye Tamasha la Michezo kwa wanawake lililoandaliwa na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka. 
    Akihutubia kwa niaba ya Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Jenista ameeleza kuwa Serikali ina mipango thabiti ya kuboresha sekta ya michezo hivyo ni wakati muafaka kwa wanawake wa rika zote kushiriki kwenye michezo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla. 
    "Wanawake tunaweza tusisubiri kuwezeshwa tujitokeze kwenye michezo kuanzia kwenye maeneo tunayoishi kwani itatusaidia kuimarisha afya zetu na kuepuka majanga ikiwemo UKIMWI hasa kwa wasichana kwa kuwa wanaposhiriki kwenye michezo wanaepuka kujihusisha na vitendo viovu kama ulevi na uasherati vinavyopelekea maambukizi" alisema Mhe. Jenista.
    Aidha Mhe. Jenista amelitaka Baraza la Michezo Tanzania  (BMT) kuandaa program maalum za kuhamasisha makundi mbalimbali kushiriki kwenye michezo hasa wanawake, watoto na walemavu. 
    Pia Mhe. Jenista ametoa wito kwa wadau wa michezo ikiwemo Mifuko ya Hifadhi za Jamii kushirikiana na BMT kuandaa matamasha mengi ya michezo yatakayohusisha wanachama wa mifuko hiyo ili kuimarisha afya zao na kuepuka maradhi kama Shinikizo la Damu na Kisukari yanayosababisha mifuko hiyo kutumia gharama kubwa kuwatibia kupitia fao la matibabu.
    Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa BMT Mhe. Zainab Vullu  (Mb) ameiomba Serikali kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya michezo ikiwemo kupunguza kodi kwa vifaa vya michezo vinavyoingia nchini na kuboresha mitaala ya elimu ya michezo mashuleni. 
    Tamasha hilo la michezo kwa wanawake limefanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam likibeba kauli mbiu ya mwaka huu inayosema " 50 kwa 50 ifikapo 2030, Tuongeze Jitihada, Maendeleo ya Wanawake kupitia Michezo Inawezekana".


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.