Rais wa wa Tanzania Dkt John Magufuli na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wamekubaliana kuhusu mpango wa kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka bandari ya Tanga, Tanzania hadi Uganda.
Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilomita 1,120 na mradi huo unatarajiwa kutoa ajira kwa watu zaidi ya 15,000.
Viongozi hao walikutana katika ikulu ndogo ya Arusha mara tu baada ya Rais Museveni kuwasili jijini humo kuhudhuria Mkutano wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais Magufuli alisema baada ya mkutano huo kwamba miongoni mwa mengine, wawili hao walijadiliana kuhusu kuongeza biashara ya ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda na kuzalisha ajira zaidi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Bw Museveni amezuru Tanzania, siku chache tu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini mwake.
Uchaguzi huo ulikosolewa na waangalizi wa kimataifa.
Kiongozi wa upinzani Dkt Kizza Besigye bado amezuiliwa kwake nyumbani na jana hakuweza kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Jana ilikuwa ndiyo siku ya mwisho iliyokubaliwa kikatiba kwa watu wasioridhishwa na matokeo kuyapinga kortini.
Mkutano wa leo wa viongozi wa Afrika Mashariki utakuwa wa kwanza kwa Dkt Magufuli na unatarajiwa kujadili maombi ya Sudan Kusini ya kutaka kuruhusiwa kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.
Iwapo ombi hilo litakubaliwa, jumuiya hiyo itakuwa na jumla ya watu takriban milioni 150.
Rais Magufuli amesema hatua kama hiyo itakuwa na „manufaa makubwa zaidi."
Brais Museveni kwa upande wake alieleza kuridhishwa kwake na utendakazi wa Rais Magufuli tangu kuchaguliwa kwake mwishoni mwa mwaka jana na kusema Jumuiya ya Afrika Mashariki imo katika nafasi nzuri ya "kwenda kwa kasi ya Rais Magufuli".
Miongoni mwa mengine yanayotarajiwa kutekelezwa na viongozi wa jumuiya hiyo ni uzinduzi wa pasipoti ya pamoja ya kielektroniki pamoja na vituo vya kuimarisha biashara mpakani.
Aidha, mzozo wa kisiasa nchini Burundi unatarajiwa kuzungumziwa ingawa haujaorodheshwa kama mada kuu.
0 comments:
Post a Comment