March 01, 2016

  • TRA YAWANASA WAKWEPA KODI KUPITIA KAZI ZA WASANII



    TRA YAWANASA WAKWEPA KODI KUPITIA KAZI ZA WASANII
    Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Yono Auction Mart pamoja na Jeshi la Polisi imefanya ukaguzi wa stempu za kodi katika kazi za wasanii na imefanikiwa kukamata CD na DVD za Muziki na Filamu takribani 7,780 ambazo hazina stempu za kodi kutoka kwa wasambazaji mbalimbali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

    Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Bw. Richard Kayombo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake.

    Bw. Kayombo alisema msako huo ulioanza tarehe 26/02/2016 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam umebaini ukiukwaji wa Sheria kutoka kwa wasambazaji wa kazi za wasanii zikiwemo CD na DVD za nyimbo na Filamu.

    Aidha, aliongeza kuwa sambamba na hilo kumebainika udanganyifu kutoka kwa baadhi ya wasambazaji kutumia stempu kinyume na sheria, "Kuna baadhi ya wasambazaji huweka CD ama DVD mbili kwenye kasha moja huku nakala moja ya CD/DVD ikiwa imebandikwa stempu halali ya kodi na nakala nyingine ikiwa haina stempu," alisema.

    Wakati huo huo baadhi ya CD na DVD zilikamatwa zikiwa zimedurufiwa pamoja na stepu ya kodi.

    Kwa upande wa kazi zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, baadhi ya kazi zilikamatwa kutoka nje ya nchi zikiwa hazina stempu ya kodi jambo ambalo ni kinyume cha sheria na pia hupoteza mapato ya nchi kwa ujumla.

    Bw. Kayombo ametoa wito kwa wasambazaji wa kazi za wasanii kutumia stempu za kodi kwa mijibu wa sheria na kusisitiza kwamba ni sharti wahusika wanaoingiza kazi za wasanii kutoka nje ya nchi wapate kibali kutoka Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili wapate kibali cha kubandika stempu kwenye kazi hizo na si vinginevyo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.