Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bado haijafunga vifaa vya kupimia joto ili kubaini dalili za awali za wagonjwa wa ebola kwenye viwanja vya ndege licha ya ugonjwa huo kuenea kwa kasi.
Awali wizara hiyo ilisema ingefunga vifaa hivyo haraka kwenye viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Mbeya.
Akizungumzia suala hilo jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kebwe alisema ununuzi wa vifaa hivyo maarufu kama thermal scanners uko kwenye mchakato wa manunuzi.
"Ununuzi wa vifaa hivi uko kwenye mchakato wa manunuzi, kama unavyofahamu Serikali inaponunua vifaa vya lazima ifuate utaratibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi wa Umma," alisema Kebwe.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba wanapata vifaa bora vinavyofanana na thamani ya fedha za watanzania.
"Wananchi wasiwe na wasiwasi vifaa hivi vitapatikana wakati wowote kuanzia sasa na vitafungwa kwenye viwanja vyetu vya ndege," alisema.
Kebwe alisema vifaa hivyo ni maalumu kwa ajili ya kupima joto kwa watu wanaoingia kwenye viwanja vya ndege.
Alisema wasafiri wanapobainika kuwa na joto linalozidi kiwango wanachukuliwa kwa ajili ya kupimwa ugonjwa wa ebola.
Moja ya dalili za ebola ni mgonjwa kuwa na joto kali na ugonjwa huo hauna tiba tayari umeua watu 1,065 katika nchi za Liberia, Nigeria, Guinea na Siera Leon huku watu wengine 1,975 wakiambukizwa virusi vya ugonjwa huo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Dharura na Maafa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Elias Kikwesi alisema hivi sasa nguvu zimeelekezwa kwenye mashirika ya ndege ambayo yanafanya safari katika nchi za Magharibi.
Alisema miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na Kenya Airways, Ethiopian Airways na Rwanda Air.
Kikwesi alisema wanashirikiana na wafanyakazi wa kwenye ndege ambao wamepewa mafunzo ya kubaini dalili za wagonjwa wa ebola.
"Kwa hiyo ndege inapotua tunakuwa na tumeshapewa taarifa za wasafiri wote kuhusu walikoanzia safari kwa ajili ya udhibiti,"alisema
Wakati huohuo Chama Wananchi CUF kimesema kwamba uamuzi wa kuweka kituo cha ugonjwa huo katika hospitali ya Temeke si sahihi kwa kuwa eneo hilo liko katikati ya mji na lina msongamano mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, Abdul Kambaya alisema endepo ugonjwa huo utasambaa hapo hospitalini utaathiri watu wengi zaidi na athari zake zitakuwa ni kubwa sana.
Taarifa hiyo iliyopendekeza litafutwe eneo jingine lililojitenga na watu ndiko kituo cha wagonjwa wa ebola kiwekwe ili kuzuia maambukizi zaidi kwa wasiokuwa na ugonjwa huo lilipingwa na msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mamwaja ambaye alisema kwamba wamezingatia vigezo vyote vya kitaalamu hivyo ni sehemu sahihi.
Alisema si wakati wa kuchanganya siasa na utaalamu, kwa kuwa hawawezi kueleza kila kitu wazi na kwamba kituo hicho kilichopo ndani ya hospitali ya Temeke kitaendelea kutekeleza majukumu yake kama ilivyopangwa, iwapo itabainika kuwepo kwa mgonjwa yeyote wa ebola.
chanzo: mwananchi
0 comments:
Post a Comment