August 21, 2014

  • MAPOROMOKO YA ARDHI YAUA WATU 32 JAPAN


    MAPOROMOKO YA ARDHI YAUA WATU 32 JAPAN
    Watu wapatao 32 wameuawa katika maporomoko ya ardhi katika mkoa wa Hiroshima nchini Japan.Maporomoko ya ardhi yametokea katika eneo la makaazi ya watu karibu na mlima katika vitongoji vya mji wa Hiroshima.Maporomoko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zilizonyesha kwa saa 24 kuamkia Jumatano asubuhi zikiwa sawa na kipimo cha mvua za mwezi mzima, limesema Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan.Picha kutoka eneo la tukio zimeonyesha nyumba zikiwa zimefukiwa katika matope na miamba, wakati kikosi cha uokoaji kikielekea nyumba hizo.
    Watu wengine tisa bado hawajulikani walipo, limesema shirika hilo.
    Afisa mwingine wa serikali ya mtaa katika mji huo amesema "baadhi ya watu wamechukuliwa na maji na ilikuwa vigumu kujua kwa uhakika idadi yao", Shirika la habari la AP limesema.
    Mwandishi wa habari wa BBC Rupert Wingfield-Hayes amesema wengi wa waliokufa ni watoto.
    Mmoja mwenye umri mdogo kabisa kufariki dunia katika tukio hilo ni mvulana mwenye umri wa miaka miwili, Shirika la habari la Japan, Kyodo limeripoti.
    Miongoni mwa waliokufa ni mfanyakazi wa uokoaji mwenye umri wa miaka 53 ambaye amekufa baada ya udongo kuporomoka tena, shirika la Hali ya Hewa la Japan limesema. Aliweza kuwaokoa watu watano wakati wa operesheni hiyo.
    Maporomoko hayo yamelikumba eneo la makaazi nje kidogo ya mji wa Hiroshima magharibi mwa Japan
    Mtu mmoja akiwa amesimama katika kifusi cha nyumba katika kisiwa cha Izu Oshima kusini mwa Tokyo Oktoba 16,2013
    Matope na miamba ilizikumba nyumba kadha, na kuwaacha wakijihifadhi kwenye mapaa ya nyumba.
    Wafanyakazi wa uokoaji wanawatafuta watu walionusurika lakini haijafahamika ni watu wangapi wamepotea.
    Mmoja wa walionusurika ameliambia shirika la AP: "Niliamka katikati ya usiku na njia ya sehemu ya kuelekea chumba cha maongezi ilikuwa tayari imefurika maji."
    "nilisikia sauti ya maji yakiingia, na hatimaye maji kutoka mtoni yaliingia ndani ya nyumba yangu, kwa hiyo nilichukua gari na kuondoka."
    Profesa mmoja katika chuo kikuu cha Hiroshima, JJ Walsh, ameiambia BBC kila mtu alishangazwa na kiwango cha upepo huo.
    "Watu wengi wamezoea mvua kubwa. Tuna msimu wa mvua. Lakini nafikiri kila mtu alikutwa na hali hii bila kujitayarisha kwa kiwango cha mvua iliyonyesha," amesema.
    Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amewataka maafisa wa serikali katika eneo hilo kuongeza idadi ya wafanyakazi wa uokoaji ili kuimarisha operesheni ya uokoaji".
    Mvua zaidi zinaweza kusababisha maporomoko zaidi ya ardhi, wameonya maafisa wa Mamlaka ya Hali ya Hewa.
    Sehemu kubwa ya sehemu ya kati na kusini mwa Japan ni milima, huku nyumba nyingi zikiwa zimejengwa katika miteremko mikali.
    Mwaka uliopita, kimbunga kilisababisha maporomoko ya ardhi katika kisiwa cha Izu Oshima, kusini mwa mji mkuu wa Tokyo, ambapo watu 35 walikufa.
    CHANZO:BBC


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.