Baada ya kuridhishwa na                matumizi mazuri na mafanikio makubwa ya Maktaba yao ya                kwanza waliyoifungua mwaka 2009 katika kijiji cha                Ngongongare Mkoani Arusha,  Taasisis isiyo ya kiserikali                ya The Crawford Smith Foundation yenye makazi yake nchini                Marekani na ambayo ndiyo inayosimamia mradi wa uanzishwa                na uendeshaji wa Maktaba hususani katika maeneo ya                vijijini, sasa inakusudia kujenga maktaba nyingine sita                katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
         Maktaba hiyo ya kwanza                na ya aina yake na ambayo imepewa jina la Jifundishe Free                Library, si tu inatoa huduma za vitabu vya kiada na ziada                kwa watumiaji ambao ni kuanzia wale wa shule za awali,                msingi, sekondari na hata vyuo vikuu, bali pia imekuwa                kituo ambacho kinawasaidia wanawake na vijana kujifunza                stadi mbalimbali zikiwamo za ujasiliamali, vyama ya kuweka                na kukopa, huduma za kinga ya afya, huduma za internet na                mafunzo ya ziada ambayo yamekuwa yakitolewa na wataalamu                wa kujitolea kutoka nje na ndani ya Tanzania. 
         Hayo yameelezwa na                Viongozi wakuu wa Taasisi hiyo ya The Crasford Smith                Foundation wakati walipofika na kufanya Mazungumzo na                Balozi Tuvako Manongi Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania                katika Umoja wa Mataifa. 
         Kwa mujibu wa maelezo                ya Bw. Steven Smith aliyekuwa amefuatana na Mke wake Bibi.                Judithi Smith amesema kuwa mwitikio mkubwa na matumizi                sahihi na endelevu vya Jifundishe Free Library na matokeo                mazuri ya wanafunzi katika mitihani yao, kumewafanya                watambue ni kwa kiasi gani huduma hiyo muhimu inahitaji                kusambazwa katika maeneo mengine hasa ya vijijini. Lengo                likiwa ni kuwafikia na kuwapatia huduma hiyo wasio kuwa na                uwezo wa kuipata kwa urahisi. 
         Mradi huo wa Maktaba                licha ya kutoa huduma mbalimbali, lakini umekwenda mbali                zaidi kwa kutoa ufadhili wa masomo ya Chuo Kikuu kwa                wanafunzi wanne hadi sasa. baadhi ya wanafunzi hao                wamerudi na kutoa mchango wao katika Maktaba hiyo na                jumuiya inayoizunguka. 
         Baadhi ya maeneo ambako                wanakusudia kupelea huduma hiyo muhimu ya maktaba ni                Kisarawe , Chunya , Iringa, Morogoro na Kilimanjaro. 
         Aidha wakuu hao                wameeleza kuridhidhwa kwao na Ushirikiano wanaoupata                kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Mhe.                Jakaya Mrisho Kikwete, baadhi ya Makampuni ambayo                yameonyesha nia ya kushirikia na Taasisi hiyo katika                utoaji wa huduma hiyo, na vilevile mwamko na moyo                wakujitolea wa watanzania katika maeneo wanayokusudia                kuanzisha maktaba hizo. 
        Kwa upande wake, Mhe.                Balozi Balozi Manongi aliishukuru Taasisi hiyo kwa mchango                wake mkubwa na ambao umeonyesha mafanikio na mabadiliko                makubwa kwa jamii inayohudumiwa. 
        Akasema Tanzania                inatambua umuhimu wa maktaba katika mustakabali mzima wa                elimu na mafunzo na kwamba mchango wa taasisi zisizo za                kiserikali unakaribishwa sana. 
                 Kutoka                  kushoto ni  Bw. Steven Smith,  Bi Ann Hanin, Mhe.                   Balozi   Tuvako Manongi na Bibi Judith Smith
        
0 comments:
Post a Comment