Na Magreth Kinabo- MAELEZO
Baraza la Vyama vya Siasa nchini limeamua mazungumzo ya maridhiano kati ya pande zinazokizana kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba kutokana na mvutano wa kutaka serikali mbili au tatu yaendelee kupitia kamati zitakazoundwa.
Aidha baraza hilo,limeamua kufanyike kongamano Agosti 9 na 10 mwaka huu mjini Dodoma kwa ajili ya kuangalia maslahi mapana ya taifa.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Kuga Mziray, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao kati ya baraza hilo, na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa,akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi kilichofanyika kwenye hoteli ya New Afrika jijini Dares Salaam.
Alisema katika mkutano huo, baraza hilo limepokea ripoti ya mkutano wa Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini na baadhi viongozi wa vyama vya siasa, pia limepokea ripoti ya chama kimoja kimoja, ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) Chama cha NCCR – MAGEUZI na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Aidha Mziray amesema kwamba katika mkutano huo, kuna mambo ambayo wamekubaliana na mengine hawakuafikiana.
"Baraza limeamua mazungumzo ya mariadhiano yaendelee kupitia kamati zitakazoundwa ,ambazo zitakuwa na wajumbe wachache. Baraza linawashauri wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba warudi Bungeni kwa kuwa ndio mahali pekee pa kutoa hoja na wala si sehemu nyingine," alisema Mziray.
Aliongeza kuwa anavipongeza vyama hivyo kwa kuonesha nia ya kuendelea kwa mazungumzo hayo na wameonesha imani na baraza hilo, ambapo wametaka majadiliano kupitia kamati yafanyike.
Mwenyekiti huyo akizungumzia kuhusu kongamano hilo ,ambalo litamhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete,ambaye atakayelifungua, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe . Mohammed Gharib Bilal, Marais wastaafu,wabunge,majaji, maspika, viongozi wote waliowahi kushika madaraka, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini zote.
"Lengo la kongamano hili ni kujadili hali ya kisiasa na mchakato wa Katiba Mpya. Kongamano hili ndio njia ya kutafuta maridhiano katika suala hili. Tunategemea busara za viongozi hawa zitatubadilkisha na kutuweka pamoja kwa maslahi ya taifa na kuachana na mambo ya kivyama," alisisitiza.
Aliyataja mambo ambayo, wamekubaliana kuwa yasiwepo wakati wa kuendelea kwa Bunge hilo ni kutumia lugha za matusi na kejeli.
Katika mazungumzo hayo, "Baraza limeona si rahisi kufikia muafaka kwani kila upande ulionesha kuwa Bunge hilo halina mamlaka ya kubadilisha Rasimu ya Katiba Mpya, na mwingine unadai Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha na kuboresha rasimu hiyo kwa vile suala hilo lipo kisheria kulingana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kifungu cha 25 na kanuni zinaruhusu," alisema Mziray.
Kwa upande mwingine Mziray alisema kuwa jambo lingine lilionesha ugumu ni mvutano uliopo wa kuhusu wa kuwepo kwa Serikali mbili au tatu kwa sababu ni suala la kisera za vyama na sera haibadilishwi mpaka mkutano mkuu wa chama.
0 comments:
Post a Comment