July 11, 2014

  • SERIKALI KUKOPESHA VIKUNDI 453 VYA VIJANA



    SERIKALI KUKOPESHA VIKUNDI 453 VYA VIJANA
    lindi pixMwenyekiti wa Kikundi cha Waendesha pikipiki Likotwa Manispaa ya Lindi, Bw. Maulid Said Mohamed (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi risala kuhusu kikundi hicho hivi karibuni Mjini Lindi. Mkurugenzi huyo alitembelea kikundi hicho ili kukagua jinsi kikundi hicho kinavyofanya kazi na jinsi kinavyonufaika na umoja huo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Lindi, Bw. Daniel Kanuse.
    (Picha na: Concilia Niyibitanga)

    ………………………………………………………………………
    Na: Concilia Niyibitanga – Afisa Habari Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
    Serikali inatarajia kukopesha vikundi vya uzalishaji mali vya vijana vipatavyo 453 katika mwaka wa fedha 2014/15 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
    Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alipotembelea kikundi cha Vijana waendesha pikipiki cha Likotwa kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.
    Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa vijana wanajiajiri wenyewe na kuondokana na dhana ya kutegemea kuajiriwa ikizingatiwa kuwa kila mwaka vijana wapatao milioni 1.2 huhitimu vyuo vikuu lakini wanaopata ajira za kuajiriwa ni vijana 200 tu. Amesema Bw. Kajugusi.
    Mikopo inayotolewa kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni njia ya kuwakomboa vijana kwa kuwaongezea mitaji ya kuweza kufanya shughuli za ujasiri na ujasiriamali na hatimaye kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.
    Bw. Kajugusi amekipongeza Kikundi cha Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda cha Likotwa kwa juhudi na mafanikio waliofikia hadi sasa kutokana na kuunda kikundi hicho chenye lengo la kuboresha maisha ya waendesha pikipiki hao.
    Aidha, amewataka kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuzingatia maadili mema ili kuimarisha amani na mshikamao katika sehemu wanazoishi na vile vile kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kama vijana wa kulipa kodi.
    Halikadhalika, amekitaka kikundi hicho kuwahamasisha vijana wenzao kushiriki katika shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru na kuwaeleza manufaa ya mbio hizo na kuwapuuza wanobeza Mwenge kwani wanaoubeza ni watumwa kwani wanaibeza historia ya nchi yao.
    Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Bw. Maulid Said Mohamed amesema kuwa kikundi kina wanachama 13 na pikipiki 2 zinazomilikiwa na kikundi na hadi sasa wameshapatiwa viwanja 6 na Uongozi wa Manispaa kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ya Kikundi.
    Bw. Mohamed amesema kuwa mpaka sasa kikundi kimejiwekea akiba na lengo kuu ni kuanzisha SACCOS kwa ajili ya kuwakopesha vijana kwa riba nafuu na hatimaye kutengeneza ajira kwa vijana wengi zaidi.
    Kikundi cha Waendesha pikipiki Likotwa kina wanachama 13 na kilianzishwa kwa nia ya kusaidiana na kujiinua kiuchumi na kina malengo ya kuanzisha SACCOS kwa ajili ya kukopesha vijana mikopo yenye masharti nafuu.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.