Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars inatarajia kutua nchini kesho (julai 6) mwaka huu ikitokea nchini Botswana ili kuendelea na programu nyingine ya mazoezi.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliweka kambi ya wiki mbili, mjini Gaborone kwa ajili ya kujiwinda na mechi dhidi ya Msumbaji kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika, AFCON mwakani nchini Morocco.
Mechi hiyo muhimu kwa kocha wa Stars, Mholanzi, Mart Nooij itapigwa katika dimba la Taifa, julai 20 mwaka huu na wiki mbili baadaye mchezo wa marudiano utapigwa mjini Maputo nchini Msumbiji.
Ikiwa ni sehemu ya kujipima ubavu, Stars ilicheza mechi ya kirafiki siku za karibuni na wenyeji wao Botswana na kuchapwa mabao 4-2.
Mabao ya Taifa stars yalifungwa na Khamis Mcha `Vialli` na John Raphael Bocco `Adebayor`.
Hata hivyo, matokeo hayo yalimfanya kocha Nooij ajue makosa ya kikosi chake na kuyafanyia kazi kabla ya kukabiliana na Black Mambas.
Katika kambi ya Gaborone, Taifa stars ilimkosa winga wake machachari, Mrisho Khalfan Ngassa `Anko` aliyesafiri kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Free State Stars inayoyoshiriki ligi ya Afrika kusini.
Kocha Nooij alimuita Ngassa ili acheze mechi ya kirafiki na Botswana, lakini ilielezwa kuwa nyota huyo alikaidi na kwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo inayonolewa na Mbelgiji Tom Saintfiet.
Taarifa za uhakika zinasema kuwa Nooij amemuengua Ngassa kuelekea mchezo dhidi ya Msumbiji na tayari nyota huyo yupo nchini baada ya kumaliza majaribio yake Afrika kusini ambapo alifuzu, lakini uhamisho wake bado ni tatizo.
Msumbiji wana historia ya kuiharibia Taifa stars katika mechi muhimu, hivyo ni muhimu kwa kocha kukisuka kikosi chake pamoja na watanzania kuisapoti timu yao.
Stars ilifanikiwa kufuzu raundi ya pili ya hatua ya awali baada ya kuifunga Zimbabwe bao 1-0 katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam na kulazimisha sare ya 2-2 mjini Harare nchini Msumbuji.
Msumbuji wao walishinda mabao 5-0 mjini Maputo na kutoka suluhu pacha ya bila kufungana dhidi ya Sudani Kusini ugenini.
Mshindi wa jumla katika mechi hiyo atafuzu hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza AFCON mwakani nchini Morocco.
0 comments:
Post a Comment