Julius Mtatiro
SIRI ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba kufanya mabadiliko kwenye kurugenzi zake kwa kumng'oa Julius Mtatiro kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, imefichuka.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya chama hicho, vinadai kuwa sababu ya kwanza imetokana na viongozi wakuu wa chama hicho taifa kumtaka Mtatiro asigombee nafasi yoyote.
Inaelezwa kwamba Mtatiro aliandaliwa kisaikolojia kwamba hatarudi kwenye nafasi yake kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Sababu ya pili ambayo inatajwa na baadhi ya viongozi wa CUF ni kwamba kiongozi huyo kijana, anadaiwa kujihusisha na matumizi mabaya ya fedha hasa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga.
Kwa mujibu wa habari hizo, sababu ya tatu inaelezwa kuwa Mtatiro alikuwa akifanya siasa za kitoto (siasa nyepesi), zilizokuwa zinawakera baadhi ya viongozi wa juu wa CUF.
"Mtatiro sio kama amependa mwenyewe kuacha nafasi hiyo la hasha, ukweli ni kwamba aliandaliwa kisaikolojia kuwa nafasi hiyo hatoshi na inamlazimu atoke ampishe Sakaya ambaye anaweza akasukuma gurudumu hilo la chama," kilieleza chanzo cha habari hizo.
CUF imefanya mkutano mkuu na kuwachagua wajumbe wapya wa Baraza Kuu pamoja na kurugenzi.
Katika mabadiliko hayo, nafasi ya Mtatiro inachukuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya.
Nafasi ya Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, imeshikiliwa na Joran Bashange, Mkurugenzi wa Haki na Binadamu na Sheria imeshikiliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Rufiji, Rukia Mchuchuli huku nafasi ya Kurugenzi ya Mipango na Uchaguzi imeenda kwa Shaweji Mketo.
Wapinga mabadiliko
Baada ya kufanya mabadiliko hayo, baadhi ya wanachama wamejitokeza kupinga uteuzi huo na leo wanatarajia kufanya maandamano ya amani kwa lengo la kuonana na kuzungumza na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba kueleza sababu za kutoridhishwa na baadhi ya viongozi.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Ibrahimu Nanga, ambaye ni mmoja wa wanachama wanaopinga uteuzi wa baadhi ya viongozi, alisema watakwenda kuwataka viongozi kuwapa fursa ya kueleza dukuduku lao.
"Lengo si maandamano bali ni kutaka kukutaka na mwenyekiti. Tunapinga uteuzi wa Shaweji Mketo na wengine waliorejeshwa wakati kipindi kilichopita hawakukisaidia chama," alisema Nanga.
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment