July 07, 2014

  • SERIKALI YARUHUSU UVUVI WA SAMAKI ZIWA RUKWA WILAYANI CHUNYA


    SERIKALI YARUHUSU UVUVI WA SAMAKI ZIWA RUKWA WILAYANI CHUNYA
    Serikali wilayani Chunya imeruhusu uvuvi katika Ziwa Rukwa kwa kipindi cha Miezi mitano baada ya kufungwa kwa miezi sita iliyopita kutokana na kupungua kwa samaki.
     Mgeni Rasmi  Afisa Tarafa ya Kiwanja, Shila Sheyo, aliyemwakilisha  Mkuu wa Wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro akiongea na wananchi
    Julius Ngwita, Afisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya, akimkaribisha mgeni rasmi
    Diwani wa Kata ya Mbangala,Abraham Sambila
    Baadhi ya wananchi wakimsikiliza mgeni rasmi




    HATIMAYE Serikali wilayani Chunya imeruhusu uvuvi katika Ziwa Rukwa kwa kipindi cha Miezi mitano baada ya kufungwa kwa miezi sita iliyopita kutokana na kupungua kwa samaki.


    Uvuvi katika ziwa hilo umeruhusiwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu hadi Desemba 31 mwaka huu Ziwa litakapofungwa tena ili kuongezeka kwa samaki kuzaliana.


    Sherehe za uzinduzi huo zilifanyika juzi katika Forodha ya Mbagala Kata ya Mbangala iliyopo Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Afisa Tarafa ya Kiwanja, Shila Sheyo, aliyemwakilisha  Mkuu wa Wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro.


    Afisa Tarafa ya Kiwanja, Shila Sheyo, alisema zoezi la kufunga ziwa hilo litakuwa endelevu ili kuwafanya samaki wazaliane na kuleta tija kwa wavuvi na uchumi kwa wananchi wanaolizunguka ziwa Rukwa.


    Alisema kufungwa kwa Ziwa hilo kunatokana na  wananchi  kuvua bila utaratibu kwa kutumia nyavu za makokolo na vyandarua hali inayosababisha  kuharibu mazalia ya samaki.


    Alisema  kitendo cha kuruhusu shughuli za uvuvi hakumaanishi kuhalilisha kwa uvuvi haramu kwani Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa watu wote watakaokiuka utaratibu.


    Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya,Julius Ngwita, ambaye pia ni Afisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya, alisema  Forodha ya Mbangala ndiyo itakayotumika kupokelea Maboti na Mitumbwi kutoka maeneo yote ya wilaya ya Chunya kwani hapo ndiyo katikati ambapo Serikali imejenga nyumba ya Afisa Uvuvi Kanda iliyogharimu zaidi ya shingi milioni sitini zilizotolewa na Serikali.

    Alisema  kila Mvuvi atatakiwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kukata leseni ya biashara,uchuuzi na vyombo vya majini kama mitumbwi na Maboti ili kuhakikisha Serikali inapata mapato.


    Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mbangala,Abraham Sambila,mbali na kuipongeza serikali kuruhusu kutumika kwa forodha hiyo na kuahidi kusimamia ipasavyo ili kudhibiti mapato yatokanayo na shughuli hizo.


    Alisema fedha zitakazopatikana hapo zitasaidia kuleta maendeleo katika Kata yake na Serikali kwa ujumla ambapo pia aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za serikali.


    Aidha ameutaka uongozi wa Kijiji kupima viwanja kwa utaratibu na wananchi wanufaike na mapato hayo ya mauzo ya viwanja na kuongeza mapato ya kijiji na Halmashauri  ya Wilaya kutokana na viwanja hivyo badala ya kugawa kiholela.


    Mwisho.

    Na Mbeya yetu





  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.