ASKOFU mkuu wa Kanisa la Assemblies Of God Tanzania (TAG) Dk. Barnabas Mtokambali, amewataka waumini na watumishi wa kanisa hilo kutumia kituo cha Redio Ushindi kueneza injili. Kauli hiyo ilitolewa jana wakati wa kuwekwa Wakfu kwa kituo cha Redio cha Ushindi kinachomilikiwa na TAG kilichopo Isyesye Jiji na Mkoa wa katika hafla iliyofanyika katika Studio za redio hiyo ambapo Askofu huyo aliwakilishwa na Makamu wake Dk. Magnus Mhiche. Akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu, Dk. Mhiche alisema kituo cha REDIO Ushindi ni kama chombo ambacho wachungaji wanaweza kukitumia kuvuna waumini na kueneza injili kirahisi kuliko kutembea kwa mguu kuwafuata waumini. Alisema redio huwafikia watu wengi zaidi bila kujali mazingira walipo hivyo ni kama kanisa linalotembea ambalo linaweza kusaidia harakati na mkakati wa kanisa wa kuwavuta waumini wengi hatimaye kuongeza idadi ya wafuasi wa kanisa la TAG tofauti na ilivyo sasa. Aidha aliwataka wafanyabiashara na watu mbali mbali kutumia kituo hicho kutoa matangazo ya biashara zao pamoja na huduma ili kuendelea kuunga mkono huduma zinazotolewa na redio hiyo ili iweze kujiendesha na kuendelea kuwepo. Hata hivyo Askofu huyo aliwaagiza wasimamizi wa Redio hiyo kutopokea matangazo yasiyokuwa na maadili ya kidini kwa madai ya kujali fedha kuliko kuangalia maudhui ya tangazo lenyewe kama linakiuka miiko ya kanisa. " Nitumie nafasi hii kuwaagiza wasimamizi wa redio sio kila tangazo linatakiwa kupokelewa hapa angalieni maadili matangazo ya madawa ya kienyeji au pombe hayatakiwi ni bora tukakosa fedha kabisa" alisisitiza Askofu huyo. Kwa upande wake Meneja wa Redio hiyo, Mathew Sasali, alisema kituo hicho kilifunguliwa Juni 1, 2011 hivyo hadi kuwekwa wakfu kinatimiza miaka 3 na sherehe hizo ni sambamba na maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa la TAG nchini Tanzania. Aidha katika Risala ya Kituo hicho iliyosomwa na Mhariri Mkuu wa Redio Ushindi, Robin Ulikaye, ilisema baadhi ya mafanikio waliyoyapata ni pamoja na kuongeza idadi ya wasikilizaji, kueneza injili kupitia Redio pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watumishi kutoka 6 hadi 13 sasa. Mwisho. Na Mbeya yetu |
0 comments:
Post a Comment