Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP Lwitiko Norman Kibanda, akizungumza na madereva wa pikipiki za kubeba abiria ambao juzi waliandamana hadi kwenye kituo hicho wakipinga kutozwa fedha sh22,000 na maofisa biashara wa wilaya hiyo, waliodai kuwa tozo hizo ni amri ya Mamlaka ya Usafirishari wa vyombo vya usafiri wa majini na nchi kavu (Sumatra).
Madereva wanaoendesha pikipiki 800 wa kubeba abiria, maarufu kama bodaboda wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiaro Mkoani Manyara, wameandamna hadi kituo cha polisi Mirerani, wakipinga kitendo cha maofisa biashara wa wilaya hiyo kuwataka walipe sh22,000 za tozo la Mamlaka ya usafirishaji wa vyombo vya majini na nchi kavu nchini (Sumatra).
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, ASP Lwitiko Kibanda, waendesha bodaboda hao walidai kuwa wamechoshwa kunyonywa na maofisa biashara hao kwani tozo hizo hutolewa eneo hilo peke yake hivyo wao wanagoma kulipa kwani wanaonewa na hawapo yatari kulipa kiasi hicho.
Mmoja kati ya madereva hao Rashid Omary alisema maofisa biashara hao waliwaeleza suala hilo siku moja na kesho yake wakaanza zoezi la kukamata pikipiki zao ili hali hawakupatiwa elimu wala kushirikishwa kwenye suala hilo, hivyo hawapotayari kulipa kiwango hivyo kwani wamechoka kunyonywa kila mara.
"Tunashangazwa kuambiwa tutoe sh22,000 za Sumatra ili hali maeneo mengine ya Arusha, Kilimanjaro au wilaya ya Simanjiro kule Landania, Orkesumet na Naberera hawalipishwi, kama sheria ya kunyoa nywele watu wote imepitishwa kwanini sisi tuwe na vipara wengine wawe na nywele, hatukubali kulipa hizo fedha," alisema Omary.
Naye, Geofrey John alisema wabunge walifuta tozo za pikipiki za kubebea abiria hivyo wanashangazwa na maofisa biashara wa wilaya hiyo kuwataka walipe fedha hizo, hivyo watagoma kutoa fedha hizo kwani hivi sasa kila mmoja anatambua haki zake na hawatakubali kuburuzwa tena.
Kwa upande wake, Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, ASP Lwitiko Kibanda aliwaeleza waendesha bodaboda hao kuwa wanatakiwa wakutane tena na maofisa biashara hao ili kuzungumzia suala hilo kwani kodi ya Serikali ni lazima ilipwe.'
"Tatizo ni kutotolewa kwa elimu juu ya suala hili kwani wengine waendesha bodaboda siyo mali zao ni waajiriwa hivyo, tujipange upya kwa maofisa biashara na ninyi bodaboda tukutane na viongozi wenu ili mueleze ipasavyo na mshirikishwe kutokana na jambo hili," alisema Kibanda.
Hata hivyo, Ofisa biashara wa wilaya ya Simanjiro, Peter Sanga alisema wanatoza sh22,000 za Sumatra wilayani humo, kwa pikipiki inayosafirisha abiria yenye magurudumu mawili na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) na texi kwa mujibu wa sheria ya Bunge.
"Tozo hiyo ni halali kulipwa na hudumu kwa muda wa mwaka mmoja na endapo mtu akilipia mwezi Mei au Julai mwaka huu, atatakiwa kulipa tena mwakani mwezi Mei au Julai na siyo vinginevyo, hivyo waendesha pikipiki za kubebea abiria ni lazima walipie pikipiki hiyo,"alisema Sanga.
Alisema Bunge halikufuta tozo hizo, kwani waliziachia na pia ada ya zimamoto kwenye pikipiki zinazolipiwa sh10,000, bima ambayo hutozwa wastani wa sh50,000 na sh22,000 ya ada ya Sumatra na ombi la kukatiwa tozo hiyo, hivyo pikipiki za kubebea abiria zinatakiwa kulipa fedha hizo za Serikali.
0 comments:
Post a Comment